1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Raia 13,000 waingia Uganda wakikimbia mapigano ya M23

29 Machi 2022

Zaidi ya wakongo 13,000 wamekimbilia nchini Uganda na kusababisha changamoto kubwa kwa wakuu wa wilaya ya Kisoro kwenye makutano ya mipaka ya Uganda, Rwanda na DRC.

Afrika Flucht Flüchtlinge in DR Kongo
Picha: Getty Images/AFP/P. Moore

Wilaya hiyo imelazimika kusitisha masomo katika baadhi ya shule ili kutoa makazi kwa watu hao huku shirika la Umoja wa Mataifa UNHCR likianzisha mipango ya kutoa misaada na huduma za dharura kwa watu hao. Japokuwa hali imekuwa tulivu kidogo ikilinganishwa na usiku wa kuamkia Jumatatu, bado raia wa nchi hiyo  wanazidi kumiminika Uganda wakielezea kuhofia usalama wao endapo watabaki ncini mwao.

Je, M23 inaibuka tena?

This browser does not support the audio element.

Kulingana na wakimbizi hao, wanadai mapigano yalizuka usiku wa kuamkia Jumatatu, baada ya wapiganaji wa M23 kushambulia vituo vya majeshi ya serikali. Idadi kubwa ya wakimbizi hao ambao ni wanawake na watoto wamekabiliwa na hali ngumu ya uhaba wa chakula, na mahitaji mengine ya msingi.

Shirika la umoja mataifa linalowashughulikia wakimbizi UNHCR limesema wimbi hili jipya la ghafla linawaweka katika hali ngumu ya kutimiza majukumu yao kwa wakimbizi hao.Uganda yalazimika kuwapokea wakimbizi 4000 wa DRC

Hofu nyingine walio nayo wakazi wa mji huo wa Bunagana ni kuzuka kwa magonjwa kutokana na msongamano wa watu ambao umeongeza shinikizo kwa miundombinu kama vile vyoo na vyanzo vya maji.

Wakati mapigano hayo yakizuka, majeshi ya DRC pamoja na majeshi ya Uganda wanaendelea na operesheni ya Shuja maeneo ya Ituri. Operesheni hiyo iliyoanza kwa vishindo mwezi Novemba ilitarajiwa kukamilika mara moja, lakini haionyeshi dalilia za kumalizika hivi karibuni, wakati ambapo waasi wakionekana kuyashugulisha zaidi majeshi ya nchi hizo mbili na kusababisha vifo vya raia wasio na hatia.