1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Raia na wanajeshi wauawa Idlib

3 Februari 2020

Takribani raia 14 wameuawa kufuatia mashambulizi yaliyofanywa na serikali ya Syria kwa kushirikiana na Urusi katika jimbo la kaskazinimagharibi mwa Syria la Idlib.

Konflikt in Syrien
Picha: picture-alliance/dpa/A. Alkharboutli

Kulingana na shirika linalofuatilia haki za binadamu nchini Syria lenye makao yake Uingereza, watu wanane wameuawa kwenye mji wa Sarmin, na saba kati yao ni wa familia moja. Kulingana na shirika hilo baba wa familia hiyo alishuhudia miili ya wanawe wawili ikifukuliwa kutoka kwenye kifusi.

Wizara ya ulinzi ya Uturuki imethibitisha kwenye taarifa yake kuhusu kuuawa kwa wanajeshi wake wanne na wengine tisa wamejeruhiwa.

Wizara hiyo imesema majeshi ya Uturuki yalijibu mashambulizi hayo kwa kuyashambulia makambi yaliyoko katika jimbo la Idlib na kuyatuhumu majeshi ya Syria kwa kuyashambulia kwa makusudi makambi yake wakati yalipofanya mashambulizi ya awali.

Mashambulizi yanayoungwa mkono na Urusi yanayolenga kulikamata moja ya eneo la mwisho la upinzania dhidi ya serikali ya mjini Damascus, yamesababisha vifo vya mamia ya raia huku watu 388,000 wwakipoteza makaazi yao mkoani Idlib.

Mamia ya raia wa Syria hii leo wamefanya maandamano ya ishara katika mji wa Harem, uliopo karibu na mpaka wa Uturuki wakishinikiza kuruhusiwa kuvuka mpaka na kuingia Uturuki. Mohammed Khitab alisikika akilalama, "Tumelazimika kuziacha nyumba zetu, watoto wetu, familia, mali, na maisha yetu, ili twende mahali ambako hata hatupajui kama Berlin."

Magari ya kijeshi ya Uturuki na malori ya mafuta yakipita kwenye mji wa Dana nchini Syria jana. Picha: AFP via Getty Images

Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, maelfu ya waasi wenye itikadi kali wamehamishwa kutoka kwenye maeneo mbalimbali ya mapambano na kupelekwa Idlib, kama sehemu ya makubaliano ya kusitisha mapigano yanayoungwa mkono na serikali. Hatua hiyo imesababisha Idlib kuwa ngome ya mwisho ya upinzani kwa Rais Bashar al Assad pamoja na kuweka mazingira mazuri ya kujiimarisha kwa makundi ya itikadi kali.

Maafisa wa Ujerumani wameiomba Urusi na Syria kumaliza mashambulizi hayo, huku waziri wa mambo ya kigeni Heiko Maas akisema hali ya kiutu katika eneo hilo la Idlib tayari ni janga kubwa na inazidi kuwa mbaya kutokana na mashambulizi hayo.

Mashuhuda wamesema idadi kubwa ya wanajeshi hapo jana imeingia kwenye eneo hilo linalodhibitwa na waasi na kuongeza kuwa kuna uwezekano kwamba wanaelekea kusini mwa jimbo la Idlib.

Wakati shirika hilo la haki za binaadamu likidai kiasi magari 40 ya jeshi hilo yalivuka na kuingia eneo la kaskazini mwa Syria mapema jana, wakati mashuhuda wengine walisema waliona magari zaidi ya 100. Uturuki ina wanajeshi waliopo kwenye vituo maalumu 12 katika mji wa Idlib vinavyofuatilia usitishwaji wa mapema wa mapigano.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW