1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Raia ni 70% ya waliouawa Gaza - Umoja wa Mataifa

8 Novemba 2024

Umoja wa Mataifa unasema takribani 70% ya waliouawa kwenye vita vya Gaza ni wanawake na watoto, huku kukiwa na ishara za wazi za uvunjwaji wa sheria za kimataifa za kuwalinda raia katika maeneo ya migogoro.

Nahostkonflikt Gaza 2024 | Luftangriff auf Wohngebäude in Beit Lahia
Picha: AFP

Umoja wa Mataifa ulilaani siku ya Ijumaa (Novemba 11) ongezeko kubwa la idadi ya raia wanaouawa kwenye vita vya Israel katika Ukanda wa Gaza, ukisema wanawake na watoto wanakaribia 70% ya maelfu ya vifo ulivyoweza kuvithibitisha.

Ofisi ya Haki za Binaadamu ya Umoja wa Mataifa ilisema ilikuwa imeweza kuthibitisha vifo 8,119 kati ya zaidi watu 34,500 waliouawa ndani ya kipindi cha miezi sita ya mwanzo ya vita hivyo ambavyo kwa sasa vinaingia mwezi wake wa 13, na kugunduwa kuwa takribani 70% ya waliouawa walikuwa wanawake na watoto. 

Soma zaidi: Marekani yasema Israel kuongeza kivuko kuingiza misaada Gaza

Athari za mashambulizi ya Israel kwenye kitongoji cha Bait Lahiya katika Ukanda wa Gaza.Picha: AFP/Getty Images

Kwa mujibu wa wizara ya afya kwenye Ukanda wa Gaza, ambao uko chini ya kundi la Hamas, kufikia mwanzoni mwa mwezi wa Novemba 2024 waliokwisha kuuawa walikuwa wanapindukia 43,000. 

Ripoti yenye kurasa 32 iliyosambazwa na Umoja wa Mataifa ilionesha kuwepo kwa "uvunjwaji wa kimfumo wa misingi mikuu ya sheria ya kimataifa." 

"Ni jambo la lazima kufanya uchunguzi wa kina kwa tuhuma nzito za uvunjwaji wa sheria ya kimataifa kupitia vyombo vya kuheshimika vya kisheria. Kwa sasa taarifa na ushahidi wote unakusanywa na kuhifadhiwa." Alisema mkuu wa Kamisheni ya Haki za Binaadamu ya Umoja huo, Volker Turk.

Muhanga mchanga, mkongwe zaidi

Kwa mujibu wa uchunguzi huo wa Umoja wa Mataifa, raia mwenye umri mdogo kabisa kuuawa na mashambulizi ya Israel kwenye Ukanda wa Gaza ni mtoto wa kiume mwenye umri wa siku moja na mwenye umri mkubwa kabisa alikuwa bibi mwenye umri wa miaka 97. 

Hali ya kitongoji cha Bait Lahia kwenye Ukanda wa Gaza kufuatia mashambulizi ya Israel.Picha: Khalil Ramzi Alkahlut/Anadolu/picture alliance

Kwa ujumla, watoto ni 44% ya wahanga wa mauaji hayo, ambapo wale wenye umri wa kati ya miaka mitano na tisa wakiwa wengi zaidi, wakifuatiwa na wenye umri wa miaka 10 hadi 14, kisha wenye umri wa juu ya hapo na hata wale wa chini ya miaka minne.

Soma zaidi: Beirut yapigwa tena huku Israel ikitanua operesheni Gaza

Matokeo ya uchunguzi huu yanaakisi mjengeko wa kiumri wa wakaazi wa ukanda huo na pia kushindwa kwa makusudi kuchukuwa hatua za hadhari kuepuka vifo vya raia. 

Hali ya kiunga cha Jabalia kwenye Ukanda wa Gaza baada ya mashambulizi ya Israel.Picha: Stringer/REUTERS

Ripoti hiyo ilionesha pia kwamba katika 88% ya vifo, watu watano ama zaidi waliuawa kwenye shambulizi moja, ikiashiria matumizi ya silaha za jeshi la Israel zenye athari kwa eneo kubwa zaidi, ingawa kwenye baadhi ya matukio inawezekana kwamba walipoteza maisha kutokana na makosa ya makombora ya wanamgambo wa Kipalestina

Hakukuwa na tamko la haraka kutoka Israel, ambayo imekuwa ikisema kuwa inachukuwa hadhari kubwa sana kuepuka kuwadhuru raia kwenye vita vyake dhidi ya kundi la Hamas katika Ukanda wa Gaza. 

Jeshi la Israel linadai kuwa kwa wastani raia mmoja ameuawa kwa kila mpiganaji mmoja wa kundi hilo, ikiliwalaumu Hamas inaodai inatumia maeneo na miundombinu ya kiraia, madai yanayokanushwa vikali na kundi hilo.