1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Raia wa Brazil wapiga kura katika uchaguzi mkuu

Zainab Aziz Mhariri: Bakari Ubena
2 Oktoba 2022

Raia wa Brazil wamepiga kura katika uchaguzi wa rais wenye ushindani mkubwa kati ya Luiz Inacio Lula da Silva rais wa zamani wa Brazil na anayetetea kiti cha urais, Jair Bolsonaro.

Brasilien | Wahlen 2022
Picha: EVARISTO SA/AFP/Getty Images

Luiz Inacio Lula da Silva ameahidi kwenye kampeni zake kwamba atairejesha Brazil katika hali ya kawaida na wakati huo huo kuna hofu kwamba mgombea wa siasa kali za mrengo wa kulia rais Jair Bolsonaro hatakubali kushindwa hali inayozusha hofu ya kuzuka mgogoro wa kitaasisi au pia ghasia za baada ya uchaguzi.

Katika uchaguzi wa leo watachaguliwa pia Wabunge, Maseneta na Magavana huku matokeo ya awali yakitarajiwa kufahamika baadaye leo.

Luiz Inacio Lula da Silva rais wanzamani wa Brazil katika kampeni.Picha: Allison Sales/FotoRua/NurPhoto/picture alliance

Uchaguzi huo umeligawa taifa hilo linaloongoza kiuchumi Amerika ya Kusini. Lula amemshutumu Bolsonaro kwa kuhusika na mauaji ya halaiki kwa sababu ya kusitasita kwake kwenye sera ya kupambana na maambukizi ya corona, huku Bolsonaro akimwita Lula kuwa ni mwizi kutokana na huyo rais wa zamani kuhukumiwa kwa kwa makosa ya rushwa na alifungwa jela.

Takriban wafuasi watatu wa Lula wameuawa na watu wanaoshukiwa kuwa wafuasi wa Bolsonaro katika miezi ya hivi karibuni. Wafuasi wa rais aliye madarakani wametoa wito mara kwa mara yafanyike mapinduzi ya kijeshi.

Rais wa Brazil Jair Bolsonaro katika kampeni za uchaguzi wa rais.Picha: Marcelo Chello/AP/picture alliance

Katika miaka yake minne ofisini, Bolsonaro ameitenga kwa kiasi kikubwa nchi ya Amerika ya Kusini kimataifa, akikataa mapendekezo ya kulinda msitu mkubwa wa Brazil na yeye mwenyewe alijizuia kusafiri nje ya nchi.

Alipopiga kura yake katika mji wa São Bernardo do Campo, Lula amekiri kutokea mabadiliko makubwa katika maisha yake baada ya kuhukumiwa katika makosa ambayo amesema yamechochewa kisiasa.

Bolsonaro alipiga kura yake katika mji wa Rio, na amesema anatarajia kushinda uchaguzi katika duru ya kwanza licha ya matokeo mabaya katika kura za maoni. Amesema hawaamini wanaoendesha kura za maoni akisema matokeo yao huwa hayaendani na uungwaji mkono aliouona kwenye kampeni zake.

Kushoto: Rais wa Brazil Jair Bolsonaro. Kulia: rais wa zamani Luiz Inacio Lula da Silva.Picha: AFP

Zaidi ya watu milioni 156 wanastahili kupiga kura katika uchaguzi wa rais. Wabunge, maseneta na magavana pia wanachaguliwa. Kupiga kura ni jambo la lazima nchini Brazil.

Iwapo hakuna hata mgombea mmoja wa urais atakayepata zaidi ya asilimia 50 ya kura katika duru ya kwanza, wagombea wawili wenye kura nyingi watakutana kwenye duru ya pili Oktoba 30.

Vyanzo: AFP/RTRE/DPA

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW