1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Cuba waanza kujadili Katiba

13 Agosti 2018

Raia wa Cuba wameanza kujadili katiba mpya ambayo inaondoa kipengele kinachoitaja Cuba kuwa taifa la kikomunisti, kutambua haki ya umiliki binafsi wa mali na inayoweka njia kuelekea kutambuliwa kwa ndoa za jinsia moja

Kuba Juan Manuel Santos Timochenko Waffenstillstandsabkommen FARC
Picha: picture-alliance/dpa/A. Ernesto

Duru za habari kutoka Havana zimesema raia wa Cuba watajadili na kutoa maoni juu ya Rasimu ya Katiba kupitia zaidi ya mabaraza laki moja ya umma yatakayoitishwa kote kisiwani humo na muda wa mwisho umepangwa kuwa katikati ya mwezi Novemba.

Zaidi ya nakala milioni moja za rasimu zimechapishwa na ripoti zinasema mahitaji yamekuwa makubwa kiasi nakala za rasimu zinauzwa katika maduka ya magazeti.

Kulingana na ratiba iliyotolewa mapendekezo yenye kujumuisha maoni ya umma yatawasilishwa mbele ya Bunge lenye wajumbe 33 mwishoni mwa Novemba ambao watakuwa na jukumu la kuandaa rasimu ya mwisho kabla ya kuitishwa kura ya maoni mwezi Februari mwaka 2019

Katiba mpya ambayo tayari kwa sehemu imepata uungwaji mkono wa Bunge itachukua nafasi ya katiba ya sasa ya mwaka 1976. 

Umiliki binafsi wa mali na ndoa za jinsia moja.

Kwa mara ya kwanza ikiwa itaidhinishwa katiba mpya ya taifa hilo itahalalisha umiliki binafsi wa mali kinyume na katiba iliyopo inayoweka masharti ya umiliki wa mali kuwa wa kijamaa huku serikali ikiwa na jukumu muhimu la kuzisimamia.

Picha: picture-alliance/dpa/AP Photo/ACN/A. Padron

Hata hivyo suala la uendeshaji binafsi wa biashara kama mikahawa, karakana na nyumba za wageni halijatajwa kwenye rasimu iliyotolewa na raia wana wasiwasi juu ya suala hilo ikizingatiwa zaidi ya waCuba nusu milioni wanaendeshaji shughuli za aina hiyo.

Katika hatua nyingine rasimu hiyo ya katiba hiyo itajumuisha kipengele kinachotambua ndoa kuwa baina ya watu wawili bila ya kutaja kuwa nmwanaume na mwanamke.

Maelezo hayo yanaweza kumaanisha kufungua milango ya kuruhusiwa kwa ndoa za jinsi moja katika taifa ambalo kwa muda mrefu limechukua msimamo wa kihafidhina.

Kadhalika rasimu ya katiba mpya inapendekeza ukomo wa mihula miwili ya urais na kuanzishwa kwa wadhifa wa Waziri Mkuu itakayoanzishwa pindi rasimu ya katiba itaidhinishwa.

Hatahivyo mapendekezo ya katiba hiyo yanakiacha cha cha kikomunisti kuwa na nguvu na udhibiti wa siasa wa kisiwa hicho.

Mwanzo mpya baada ya Zama za Ukomunisti?

Havana inatumai mabadiliko hayo ya katiba yaliyoasisiswa na rais aliyeondoka madarakani Raul Castro yataleta mageuzi makubwa kwa kujumuisha fikra mamboleo za ujamaa badala ya zile za ukomunisti wa zama za jamhuri ya kisovieti. 

Picha: Imago/Agencia EFE/M. Vazquez

Rais wa Cuba Miguel Diaz-Canel amewatolea wito raia kujiandaa kikamilifu ili kushiriki mikutano ya kutoa maoni na kusisitiza rasimu ya katiba ina masuala muhimu yanayohitaji uamuzi wa pamoja wa raia wa taifa hilo.

Tangu kuondoka madarakani kwa kiongozi mwanamapinduzi hayati Fidel Castro, Cuba imeshuhudiia mageuzi makubwa yanayoelekea kumaliza ushawishi wa falsala za kikomunisti kwenye taifa hilo dogo na maskini Barani Amerika.

Mwandishi: Rashid Chilumba

Mhariri: Mohamed Abdulrahman

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW