Raia wa Gambia leo wanapiga kura ya kumchagua Rais
4 Desemba 2021Rais wa sasa Adama Barrow aliyechaguliwa kwa mara ya kwanza mnamo mwaka 2016, ana matumaini ya kushinda muhula wa pili katika uchaguzi wa rais unaofanyika leo Jumamosi. Wagombea sita wanagombea kiti cha urais. Wachambuzi wanasema ushindani mkali ni kati ya wagombea wawili ambao ni Rais Adama Barrow wa chama cha NPP na aliyekuwa Naibu wake Ousainou Darboe anayegombea kwa tiketi ya chama cha United Democratic Party (UDP).
Wagombea wote wamesisitiza juu ya ajenda ya kuleta mabadiliko kwenye kampeni zao wakati ambapo raia wa Gambia bado wanaisaka haki nchini mwao, wanataka uchumi imara baada ya taifa hilo pia kukumbwa na athari zilizosababishwa na janga la corona hali ambayo inachochea idadi kubwa ya watu wanaojaribu kuikimbia nchi hiyo kwa kutumia njia za hatari kwenda barani Ulaya.
Wiki iliyopita, Tume ya Ukweli, Maridhiano na Fidia ilikabidhi ripoti yake ya kurasa 17 kwa Rais Barrow, ikimtaka kuyatekeleza matarajio katika kuhakikisha kuwa wahalifu waliokiuka haki za binadamu wanachukuliwa hatua.
Utawala wa miongo miwili wa rais wa hapo awali Yahya Jammeh ulikumbwa na vitendo vya watu kukamatwa kiholela, wengine kupotezwa bila kujulikana walikopelekwa na mauaji mambo ambayo yalifichuliwa na watu waliotoa ushuhuda wakati wa vikao vya tume vilivyoendeshwa kwa miaka kadhaa. Barrow, ameitaja tume hiyo kuwa ni moja ya mambo muhimu katika kazi yake ya urais na ameahidi kwamba wahusika watafunguliwa mashtaka na waathirika watatendewa haki.
Wafuasi wa Barrow, wameiambia DW kuwa rais Adama Barrow anapenda watu sana na hivyo wanataka kuwa naye maisha yote. Lakini kwa wakosoaji wa Barrow, rais huyo amevunja ahadi yake muhimu zaidi kwani alipoingia madarakani mwaka wa 2017, aliahidi kubakia madarakani kwa miaka mitatu pekee na sasa uamuzi wake wa kugombea tena kiti cha urais umeliweka katika darubini taifa hilo la Afrika Magharibi.
Profesa Pierre Gomez, ambaye pia ni Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Gambia, amesema misimamo ya kisiasa isipewe nafasi tena kuwagawa Wagambia.
Kulingana na mtafiti wa maswala ya siasa katika Chuo Kikuu cha Gambia ambaye pia ni mchambuzi wa maswala ya kisiasa Essa Njie, Gambia inakabiliwa na changamoto lukuki, kuanzia ukosefu wa ajira hasa miongoni mwa vijana, masuala ya afya, elimu, miundombinu, na uchumi. Njie amesema changamoto nyingine ambayo Gambia inapaswa kukabiliana nayo ni ushawishi wa aliyekuwa rais wa zamani Yahya Jameh na kuingilia kwake kati katika siasa za Gambia. Jameh, aliitawala Gambia kwa miaka 22.
Vyanzo:/AP/AFP