Wakenya hawatoandikishwa kuipigania Urusi dhidi ya Ukraine
17 Machi 2026
Tangazo hilo limetolewa na Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Kenya Musalia Mudavadi aliyekutana na kufanya mazungumzo na mwenzake wa Urusi Sergei Lavrov mjini Moscow.
Tangazo kuhusu makubaliano hayo limetolewa wakati umma wa Kenya ukiwa na hofu ya kuwepo kwa mtandao wa ulanguzi wa binadamu unaowezesha raia kupelekwa Urusi ili kupigana katika vita vya Ukraine.
Akitoa tangazo kuhusu makubaliano hayo Waziri wa Mambo ya nje wa Kenya Musalia Mudavadi aliwahakikishia Wakenya kuwa, "Nataka niweke wazi kuwa sasa tumekubaliana kwamba raia wa Kenya hawataandikishwa kupitia Idara ya Ulinzi ya wala Wizara ya Ulinzi hapa. Hawatakuwa na sifa ya kujiandikisha kwenye operesheni maalumu na tunataka kushukuru kwa hilo."
Mudavadi ameongeza kuwa huduma za kibalozi zitaratibiwa kupitia njia sahihi za kidiplomasia kwa ajili ya Wakenya wanaohitaji msaada, ambao tayari wameshajiandikisha kupigana vita upande wa Urusi.
Urusi inatambua hofu dhidi ya Kenya, itatoa ushirikiano
Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergei Lavrov licha ya kusema kuwa raia wa Kenya walisaini mikataba ya kupigana kwa hiari, amesisitiza kuwa nchi yake inatambua hofu ya Kenya na kuongeza kuwa, "Tunaelewa wasiwasi huu wa Kenya. Kama ilivyo kwa taifa lolote la kawaida, ni lazima serikali zote ziwajali raia wake. Na taarifa zozote zinazohitajika kutoka kwenye Ubalozi wa Kenya ulio Moscow kuhusiana na kila Mkenya ambaye yuko kwenye operesheni maalumu zitapelekwa haraka kwa Wizara ya Ulinzi ya Urusi."
Ripoti za Kiitelijensia za Kenya zinadai kuwa zaidi ya raia 1,000 wamepelekwa katika taifa hilo lililo mashariki mwa Ulaya kufanya kazi kwa ahadi ya mishahara ya kuvutia huku wanaokwenda kupigana wakilipwa ziada ya dola 6,000.
Idadi hiyo ni mara tano ya ile iliyokadiriwa awali na mamlaka nchini humo. Hadi sasa hakuna takwimu rasmi kuhusu ni Waafrika wangapi hasa waliojiunga na mapigano hayo kati ya Urusi na Ukraine lakini Kyiv inasema zaidi ya Waafrika 1,700 wako kwenye mapambano upande wa Urusi.
Kando ya makubaliano ya kutowachukua Wakenya kwenye mapigano dhidi ya Ukraine, Lavrov na Mudavadi wameusifu uhusiano wa nchi zao ikiwemo hatua ya iliyokuwa Umoja wa Kisovieti kuutambua uhuru wa Kenya kutoka kwa Uingereza mwaka 1963. Aidha, Mudavadi amesema Kenya na Urusi zinaweza kuongeza ushirikiano katika sekta za nishati, uchumi na kilimo.