Raia wa kigeni waanza kuondoka Gaza kuelekea Misri
1 Novemba 2023Kwa mujibu wa chanzo kimoja cha usalama kutoka Misri ni kwamba raia wa kigeni wapatao 500 watavuka kivuko cha Rafah kutoka Gaza na kuingia Misri leo Jumatano. Picha za moja kwa moja kutoka eneo hilo zimeonyesha umati mkubwa wa watu wakisubiri upande wa Palestina kwenye kivuko hicho wakikadiriwa kufikia watu 200.
Ingawa malori zaidi ya 200 yaliyokuwa yamebeba misaada ya kiutuyaliruhusiwa kuingia Gaza kutokea Misri, hakuna watu ambao waliruhusiwa kuondoka Gaza. Serikali za kigeni zinasema raia wa kutoka takribani nchi 44 pamoja na mashirika 28 yakiwemo yale ya Umoja wa Mataifa walikuwa wakiishi Ukanda wa Gaza ambako wakaazi wake wapatao milioni 2.3 wamekabiliwa na mashambulizi ya Israel kwa zaidi ya wiki tatu, katika hatua ya kujibu shambulizi la Hamas la Oktoba 7.
Mbali na raia hao wa kigeni, pia Wapalestina wapatao 90 waliojeruhiwa vibaya au wako katika hali mbaya sana ya kuumwa wanatarajia kuvuka na kupatiwa matibabu Misri. Idadi kubwa ya magari ya kubeba wagonjwa imeshuhudiwa ikisubiri katika kivuko hicho. Misri pia imesema itajenga kituo cha muda cha matibabu cha kuwapokea watu waliojeruhiwa katika mji wa Sheikh Zuweid ambao upo kilometa 15 kutoka Rafah.
Soma pia: Israel na Misri zaruhusu misaada ya kibinaadamu kupelekwa Gaza
Jeshi la Israel limesema kwamba askari wake 11 wameuawa katika mapigano ya ardhini ndani ya Gaza siku ya Jumanne, na kufanya idadi jumla ya wanajeshi waliouawa tangu Oktoba 7 kufikia 326. Askari wengine wawili walijeruhiwa vibaya katika mapigano ya Jumanne huku jeshi la Israel likidai kuyalenga zaidi ya maeneo 11,000 ya wanamgambo tangu ilipoanza vita vyake dhidi ya Hamas. Katika hotuba yake kwa taifa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ameahidi "ushindi" dhidi ya Hamas licha ya "athari za kuumiza."
"Tuko kwenye vita vikali. Vitakuwa ni vita vya muda mrefu. Tumekuwa na mafanikio makubwa lakini pia hasara chungu nzima. Wanajeshi wetu wameanguka katika vita vya haki kabisa, vita dhidi ya nyumba zetu. Na ninaahidi kwa raia wote wa Israeli tutafanya kazi hiyo. Tutasonga mbele hadi ushindi," alisema Netanyahu.
Hayo yakiendelea, Bolivia ilitangaza hapo jana kwamba inavunja uhusiano wa kidiplomasia na Israel. Katika tangazo lake naibu waziri wa mambo ya nje wa Bolivia Freddy Mamani alisema wamechukua hatua hiyo katika "kukataa na kulaani mashambulizi makali ya kijeshi na yasiyo na uwiano yanayotekelezwa katika Ukanda wa Gaza na Israel." Baadae waziri mwingine katika ofisi ya rais wa Bolivia Maria Nela Prada, naye pia alitangaza kwamba watapeleka misaada ya kiutu huko Gaza.
Janga la kiafya: Gaza kutumbukia janga la kiafya - WHO
Israel tayari imeukosoa uamuzi wa Bolivia wa kukata uhusiano wa kidiplomasia ikisema ni "kukubali ugaidi na kujisalimisha kwa utawala wa Iran". Wizara ya mambo ya kigeni ya Israel imeongeza katika taarifa hiyo kwamba "kwa kuchukua uamuzi huo serikali ya Bolivia inajifungamanisha na kundi la kigaidi la Hamas."
Bolivia limekuwa taifa la kwanza la Amerika ya Kusini kuvunja uhusiano na Israel tangu mzozo huo ulipozuka upya na kundi la Hamas.