Raia wa Misri bado wanaandamana
29 Januari 2013Ni sauti zilizosikika katika barabara moja ya ufukweni karibu na uwanja wa Tahriri mjini Cairo. Kwa siku mbili mfululizo pamekuwepo na machafuko katika eneo hili. Vijana wanarusha mawe na moto. Polisi wanarusha mabomu ya kutoa machozi. Machafuko yaliongezeka jana baada ya rais Mursi kutangaza Jumapili kwamba atachukua hatua kali zaidi kupambana na waandamanaji. Watu walioshuhudia matukio haya kwa macho wanaeleza kwamba polisi waliwafyatulia risasi za mpira wale waliotoka nje kumpinga Mursi.
Katika hotuba aliyoitoa kwenye televisheni, rais huyo amewaalika wapinzani wake kufanya mazungumzo. Hata hivyo, vuguvugu la ukombozi nchini Misri, ambalo ni muungano wa vyama vya upinzani visivyoegemea dini, vimekataa mwaliko huo. Badala yake, limetoa masharti haya: "Ni lazima rais Mursi awahakikishie raia wa Misri kwanza kwamba analipa uzito suala la mazungumzo. Hii inamaanisha kuwa anatakiwa kuwajibika kwa mauaji yaliyotokea." Anasema Hamdin Sabbahi, mmoja wa viongozi wa kundi hilo.
Lakini jambo hilo si rahisi kutokea. Kwa mtazamo wa Mursi na chama chake cha udugu wa Kiislamu, maandamano yanayoendelea yamechochewa na wahalifu na watu wenye kupenda vurugu.
Upinzani nao umegawanyika
Essam El-Erian ni naibu mwenyekiti wa chama hicho: "Rais anatekeleza tu kile ambacho wananchi wake wanakitarajia kutoka kwake. Tunategemea kwamba Mursi atapuuzia kelele za kisiasa za wapinzani. Kila anayetumia nguvu lazima awajibike mbele ya sheria. Hakuna aliye juu ya sheria, haijalishi ana mtazamo gani wa kisiasa."
Misri imegawanyika. Upande mmoja amesimama Mursi na watu wenye msimamo mkali wa Kiislamu na upinzani umesimama upande wa pili. Pande zote zinaungwa mkono na watu wengi. Hivi sasa linajitokeza kundi la tatu, ambalo ni la watu wanaompinga rais Mursi huku wakisema kuwa upinzani hauna nguvu ya kutosha na umegawanyika. Hasira ya watu hao ilionekana pia katika siku zilizopita. Inaelezwa kwamba zaidi ya majengo 50 ya taasisi za serikali na chama cha udugu wa kiislamu yaliharibiwa au kuchomwa moto.
Mohammed Mursi bado ni rais halali wa Misri. Lakini sauti za wale wanaotaka aondoke madarakani zinaongezeka. Wanaonyesha hasira zao kwa kuandamana. Kama walivyofanya jana katika miji ya Alexandria, Ismailiya, Suez na Port Said.
Mwandishi: Jürgen Stryjak
Tafsiri: Elizabeth Shoo
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman