Raia wa Misri kuandamana upya leo
28 Januari 2011Mwanasiasa muhimu wa upinzani,Mohamed El Baradei,ambaye ni kiongozi wa zamani wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Atomiki,IAEA,kwa sasa yuko nchini Misri ili kuwaunga mkono waandamanaji hao,baada ya kuuzuru mji wa Vienna ulioko Austria.Kwa mujibu wa mshindi huyo wa Tuzo ya Nobel,uongozi wa Rais Hosni Mubarak umewawia waMisri vigumu na kilichosalia ni maandamano.
Mohamed El-Baradei anaaminika kuwa mgombea mtarajiwa atakayetoa ushindani mkubwa kwa rais Hosni Mubarak katika kinyang'anyiro cha kuwania urais mwaka huu. Wafuasi wa wanasiasa wa upinzani wamekuwa wakiandamana tangu siku ya Jumanne katika mji mkuu wa Cairo na Suez,ulio bandarini ijapokuwa wamepigwa marufuku.Kwa sasa kiasi ya watu alfu moja wamekamatwa na wengine 6 wameuawa kwasababu ya purukushani hizo.