1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Raia wa Sudan bado wanapinga utawala wa kijeshi

1 Desemba 2021

Vikosi vya usalama vya Sudan vilitumia mabomu ya kutoa machozi ili kuwatawanya maelfu ya waandamanaji waliokusanyika katikati mwa Khartoum siku ya jumanne, ili kupinga utawala wa kijeshi kufuatia mapinduzi.

Sudan
Picha: Marwan Ali/AP/picture alliance

Waandamanaji hao wanayapinga pia makubaliano ya hivi majuzi ya jeshi hilo na Waziri mkuu licha ya wanasiasa waliozuliwa tangu mapinduzi hayo kuachiliwa huru. 

Hadi sasa watu 42 ndio tayari wameuawa katika vurugu hizo huku wengine kadhaa wakikamatwa. Kamati za upinzani za vitongoji ziliitisha maandamano hayo kwa kudai mamlaka kamili ya kiraia na kutupilia mbali makubaliano ya wiki iliyopita yaliomrejesha kwenye wadhifa wake Waziri Mkuu wa kiraia Abdalla Hamdok na kupelekea kuachiliwa kwa wanasiasa wakuu kadhaa waliozuiliwa tangu wakati huo wa mapinduzi.

Unyakuzi wa madaraka wa Oktoba 25 ulisitisha ushirikiano na makundi ya kisiasa ya kiraia tangu kuondolewa madarakani kwa Omar al-Bashir mwaka 2019 na kuibua shutuma kutoka kwa madola ya Magharibi, ambayo pia yalisimamisha misaada. Vikosi vya polisi wenye silaha nzitonzito vilielekea katikati mwa Khartoum, ambapo waandamanaji walipanga kuandamana hadi ikulu ya rais.

Polisi walirusha mabomu ya machozi na gruneti za kushtukiza na zenye milio mikali ya kutisha ili kuwatawanya waandamanaji waliokuwa wamezuia barabara kuu takriban kilometa moja kutoka Ikulu huku wakiimba "Nafasi ya Askari ni Kambini". 

Chama cha wataalam wa Sudan kimebaini katika taarifa yake kuwa waandamanaji kadhaa wamekamatwa huku Kamati Kuu ya Madaktari wa Sudan ikisema kuwa mwandamanaji mmoja aliejeruhiwa alikamatwa wakati akipewa matibabu katika hospitali moja wapo iliyopo karibu na sehemu ya maandamano hayo.

Kiongozi wa kijeshi Abdel Fattah al-Burhan na waziri mkuu Abdullah HamdokPicha: dpa/picture alliance

Baadhi ya wanasiasa walioachiliwa walionekana kwenye maandamano hayo.Wagdi Salih, kiongozi maarufu alieibua mzozo kuhusu Kikosi kazi cha kupambana na rushwa ambae aliachiliwa Jumatatu usiku. Waziri wa zamani wa viwanda Ibrahim al-Sheikh pia aliachiliwa Jumanne pamoja na washiriki wawili wa kikosi kazi, familia yake ililiambia shirika la habari la Reuters. Hata hivyo, Salih, Al-Sheikh na mwanasiasa mwenzake Ismail al-Tag, wanakabiliwa na mashtaka ya uchochezi wa jeshi, wakili Moiz Hadra alisema.

"Bado kuna wafungwa katika gereza la Soba huko Khartoum, wanaume, wanawake na watoto waliokamatwa wakati wa maandamano chini ya hali ya hatari na tunahimiza waachiliwe pamoja na wengine katika majimbo ya Sudan,” aliongeza.

Mtawala wa kijeshi Abdel Fattah al-Burhan amesema mapinduzi hayo yalihitajika ili kurejesha utawala wa mpito wa Sudan kwenye njia iliyonyooka na hivyo maandamano ya amani yanaruhusiwa. Al Burhan amesisitiza kuwa uchunguzi unafanywa kuhusu vifo vinavyotokea wakati wa maandamano , huku akiwalaumu polisi na makundi ya wanasiasa wenye silaha.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW