1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Raia wa Syria wakimbia Idlib wakihofia mashambulizi

Caro Robi
6 Septemba 2018

Mamia ya raia wamekimbia kutoka  vijiji vilivyo karibu na eneo la mapambano katika jimbo la Idlib wakihofia mashambulizi makali kutoka kwa wanajeshi wa serikali wanaopania kuikomboa ngome hiyo ya mwisho ya waasi.

Syrien Krieg Flüchtlinge in Idlib
Picha: picture-alliance/Anadolu Agency/M. Abdullah

Wanajeshi wa serikali ya Syria wanaoungwa mkono na Urusi wamekuwa wakijikusanya karibu na jimbo hilo la Idlib lililoko kaskazini magharibi mwa nchi kwa majuma kadhaa sasa. Jana Urusi ikifanya mashambulizi yake ya kwanza ya angani katika kipindi cha majuma matatu yaliyopita.

Wanavijiji wameyahama makazi yao na kuelekea kaskazini mwa jimbo jirani la Aleppo ambalo pia linadhibitiwa na waasi. Mkurugenzi mkuu wa shirika la kutetea haki za binadamu Syria Rami Abdel Rahman amesema karibu watu 1,000 walianza kuondoka Idlib jana jioni.

Waasi wa Syria wakijiandaa kwa operesheni ya kijeshi IdlibPicha: Getty Images/AFP/O.H. Kadour

Idlib ni ngome ya waasi

Karibu nusu ya Idlib inadhibitiwa na kundi la waasi linalojulikana Hayat Tahrir al Sham, kundi la wanamgambo wenye itikadi kali lenye mafungamano na mtandao wa kigaidi wa Al Qaeda. Nusu nyingine ya jimbo hilo iko mikononi mwa waasi wanaoungwa mkono na Uturuki. Majeshi ya serikali yaliyakomboa maeneo mengi ya kusini mashariki mwa Idlib mapema mwaka huu.

Umoja wa Mataifa umeelezea wasiwasi kuwa operesheni kali ya kijeshi Idlib huenda ikawaacha watu zaidi ya laki nane bila ya makazi. Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Syria Steffan Di Mistura ameziomba nchi zenye nguvu zaidi duniani kuingilia kati ili kuepusha kile alichokitaja umwagaji wa damu.

Hapo kesho Ijumaa, Urusi na Iran ambazo ni washirikwa wakubwa wa utawala wa Rais Bashar al Assad zinatarajiwa kufanya mkutano wa kilele mjini Tehran huku Uturuki ambayo inayaunga mkono makundi ya waasi Syria  nayo ikishiriki  na ikitarajiwa kuamua hatma ya jimbo hilo la Idlib.

Mkutano wa amani kufanyika Tehran

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa pia linatarajiwa kukutana kesho kujadili hali ilivyo Syria. Duru chungu nzima za mikutano ya kutafuta amani nchini humo zimeshindwa  kukomesha vita vya wenyewe kwa wenyewe Syria ambavyo vimewaua zaidi ya watu laki tatu na kusababisha mamilioni ya wengine kuyahama makazi yao na kuwa wakimbizi tangu mwaka 2011.

Wapiganaji wa kundi la NLF mjini IdlibPicha: Getty Images/AFP/N. Al-Khatib

Uturuki ambayo ni nchi jirani na Syria, inayowahifadhi zaidi ya Wakimbizi milioni tatu kutoka Syria inahofia kuwa itashuhudia wimbi jipya la mmmiminiko wa wakimbizi.

Waziri wa mambo ya nje wa Uturuki Mevlut Cavusoglu amesema nchi yake inataka kuepusha mashambulizi Idlib na kuongeza kuwa ameiambia Urusi kuwa ni wazi mashambulizi iliyofanya jana Jumatano Syria,haikuwa hatua sahihi.

Naye mkuu wa majeshi ya Ufaransa Francois Lecointre amesema majeshi yake yako tayari kufanya mashambulizi Syria iwapo silaha za sumu zitatumika katika operesheni ya majeshi ya serikali ya syria katika mji wa Idlib.

Lecointre amesema anatumai kuwa kundi la wanamgambo wenye itikadi kali la dola la Kiislamu IS litatokomezwa Syria na Iraq ifikapo mwisho mwa mwezi Novemba. Ufaransa imeongeza kuwa kuna ishara kuwa Urusi inataka kukamilisha operesheni ya kijeshi Idlib ifikapo mwishoni mwa mwaka huu

Mwandishi: Caro Robi/Afp/Reuters

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW