1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Raia wa Ujerumani warudisha imani yao kwa kansela Merkel

7 Oktoba 2016

 Umaarufu wa Kansela wa Ujerumani Angela Merkel umeanza kuimarika, hayo yamejiri kufwatia uchunguzi uliofanyika mwanzoni mwa mwezi wa Oktoba. Uungwaji mkono kwa Merkel ulipungua kwa miaka mitano mfululizo.

Deutschland Berlin - Angela Merkel auf dem Unternehmertag des BGA
Picha: picture-alliance/dpa/T. Brakemeier

 Asilimia 54 miongoni mwa zaidi ya watu 1000 waliohojiwa walisema kwamba wameridhika na kazi inayofanywa na bibi Merkel.  Umaarufu wake umeongezeka kwa  alama 9 kinyume na asilimia 45 za wakati uliopita kwa mujibu wa taarifa za uchunguzi uliofanyika.

Kushuka kwa umaarfu wa kansela wa Ujerumani kulisababishwa na sera zake za kuweka mlango wazi kwa wakimbizi. Uchunguzi huo uliofanywa kwa njia ya simu umechapisha pia umaarufu wa wanasiasa wengine wa ujerumani. Waziri wa mambo ya nje anayeungwa mkono zaidi hapa nchini kutoka chama cha  Social Democratic SPD Frank - Walter Steinmeier ameungwa tena mkono kwa asilimia 75 huku wananchi wa Ujerumani wakisema kuwa wanaridhishwa mno na utendaji wake wa kazi.
Wa pili ni waziri wa fedha Wolfgang Schäuble ambae umaarufu wake umefikia asilimia 63.

Wakati huo huo umaarufu wa waziri mkuu wa jimbo la Bavaria Horst Seehofer umepungua kwa alama saba na hivyo basi kuungwa mkono kwa asilimia 37 pekee. Seehofer anatoka katika chama cha CSU ambacho ni chama ndugu kinachoshirikiana na cha kansela Angela Merkel cha CDU, amekuwa mkosoaji mkubwa wa sera za bibi Merkel kuhusu idadi ya wakimbizi wanaoingia humu nchini.  Amekuwa akitaka idadi hiyo kubwa iwekewe kizuizi. Raia wa Ujerumani wamesema wanaunga mkono utendaji wake katika maswala ya kisiasa.

Kansela Merkel na mmoja wa wakimbiziPicha: Getty Images/S. Gallup

Kufuatia matokeo katika kura ya maoni ya Hungary ambapo asilimia 98 ya raia wa nchi hiyo walipinga sera ya Umoja wa Ulaya kuhusu kugawana wakimbizi, maswali yameendelea kujitokeza iwapo sera hiyo inayozihusisha nchi za Ulaya itaweza kutekelezeka? au kila nchi ijiamulie yenyewe kuhusu kiwango cha wakimbizi  itakachotaka kuwachukua.

Theluthi mbili ya raia wa Ujerumani hawana imani na mpango huo wa Ulaya wa kulishughulikia swala la wakimbizi kwa pamoja umebaini uchunguzi huo. Kuhusu namna ya kuwakaribisha wakimbizi asilimia 98 ya raia wa Ujerumani walioulizwa walisema kwamba lugha ya Kijerumani ni lazima ipewe kipaumbele katika mafunzo, vile vile watoto wahamiaji wapewe nafasi katika shule za hapa nchini kwa ajili ya kujifunza utamaduni wa Kijerumani. 

Ujerumani hivi karibuni imekabiliwa na mashambulio kutoka kwa watu wenye itikadi kali zinazolemea mrengo wa kulia ikiwa ni pamoja na mashambulio mawili ya mabomu katika mji wa Dresden. mashambulio hayo ya mabomu yalifanyika nje ya msikiti na jengine katika kituo cha kimataifa cha mikutano lakini hakuna majeruhi walioripotiwa kwenye mashambulio hayo ambayo polisi wanashuku yalihusiana na maswala ya ubaguzi.

Hata hivyo asilimia 84 ya raia wa Ujerumani wana hofu kwamba vitisho vya mashambulio yanayofanywa na makundi yanayoegemea mrengo wa kulia ndio jambo linalowatia wasiwasi zaidi.

Uchunguzi huo umefanywa na taasisi ya Infratest ambapo walioshirikishwa walikuwa ni watu ambao wamefikisha umri wa kupiga kura.

Mwandishi Zainab Aziz/APE/DW English

Mhariri:   Yusuf Saumu