1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Raia wa Urusi wapiga kura ya rais

15 Machi 2024

Raia wa Urusi wanapiga kura katika uchaguzi wa rais utakaofanyika kwa muda wa siku tatu na unaotarajiwa kumkabidhi rais Vladimir Putin muhula mwingine wa miaka sita.

Rais wa Urusi Vladimir Putin
Walinzi wa Kremlin wakifungua milango ya dhahabu kwa Rais wa Urusi Vladimir Putin katika ikulu ya Kremlin.Picha: Alexei Druzhinin/ZUMAPRESS.com/picture alliance

Vituo vya kupigia kura vilifunguliwa saa mbili asubuhi hii leo kwenye rasi ya Mashariki ya Mbali ya Kamchatka na vitafungwa Jumapili saa mbili jioni katika eneo la Kaliningrad nchini Urusi, linalopakana na Poland na Lithuania.

Katika ujumbe wa kabla ya uchaguzi uliotangazwa kwenye runinga ya serikali Putin amewataka raia wa Urusi kumuunga mkono licha ya kile alichokitaja kama "kipindi kigumu" kwa taifa hilo.

Matumaini ya kiongozi huyo wa Kremlin yameongezeka wakati wanajeshi wake hivi karibuni wakipata  ushindi wao wa kwanza kwenye uwanja wa vita huko Ukraine baada ya kipindi cha takriban mwaka mmoja.

Soma pia: Putin asifu mafanikio Ukraine, atishia vita vya nyuklia

Huku wapinzani wote wakuu wa Putin wakiwa wamekufa, wakiwa gerezani au uhamishoni, matokeo ya kura hayana shaka yoyote. Uchunguzi wa maoni ulioendesha na kituo cha televisheni cha serikali umeonesha kwamba Putin atapata zaidi ya asilimia 80 ya kura.

Ushindi huo utamruhusu kukaa madarakani hadi 2030, ukiwa muda mrefu zaidi kuliko kiongozi yeyote wa Urusi tangu Catherine the Great katika karne ya kumi na nane.

Uchaguzi huo hata hivyo unafanyika huku kukiwa na ukandamizaji mkubwa dhidi ya upinzani, vyombo huru vya habari na makundi maarufu vya haki za binaadamu na kumfungulia mlango Putin wa kuudhibiti kikamilifu mfumo wa kisiasa.

Mustakabali wa Urusi

Zoezi la upigaji kura wa mapema katika uchaguzi wa rais wa Urusi huko Mariupol inayokaliwa na Urusi.Picha: Alexander Ermochenko/REUTERS

Raia wanapiga kura kwenye vituo karibu 100,000 kuanzia (15.03.2024) hadi Jumapili ndani ya taifa hilo na kwenye maeneo yaliyonyakuliwa na Urusi huko nchini Ukraine katikati ya vita vilivyoingia mwaka wa tatu sasa.

Sergei Aksyonov, mwanasiasa wa Urusi anayehudumu kama mkuu wa  Crimea baada ya kupiga kura alisema:

"Nimepiga kura hivi punde kwa mustakabali wa Urusi. Hali ni nzuri. Ni siku nzuri. Uchaguzi unafanyika. Kila kitu kinakwenda kulingana na mpango. Tunapiga kura kwa mustakabali wa Urusi. Piga kura yako kwa mustakabali wa usalama, maendeleo ya kiuchumi, maisha na afya ya watoto na wajukuu zetu."

Mapambano yaendelea

Mabaki ya gari ambalo lilishambuliwa kwa ndege isiyo na rubani ya Jeshi la Ukraine.Picha: Pavel Kolyadin/TASS/dpa/picture alliance

Huku haya yakijiri watu wawili wamejeruhiwa katika mashambulizi kwenye mpaka wa Urusi na Ukraine karibu na mji wa Belgorod leo Ijumaa.

Kupitia mtandao wa Telegram Gavana Vyacheslav Gladkov amethibitisha tukio hilo huku Wizara ya Ulinzi ya Urusi ikisema kuwa makombora saba ya Ukraine yalivurumishwa Belgorod.

Shirika la habari la serikali Ria Novosti limeripoti kwamba watu walilazimika kuondoka kwenye vituo vya kupigia kura kutafuta hifadhi katika maeneo salama.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW