Raia wa Zimbabwe wajiandaa kupiga kura hapo kesho.
30 Machi 2005Rais Robert Mugabe, amefanya safari nyingi nchini Zimbabwe majuma machache kabla uchaguzi wa kesho. Katika kampeni yake amemlaumu waziri mkuu wa Uingereza, bwana Tony Blair, kuwa anajaribu kuleta tena ukoloni nchini Zimbabwe kwa kukiunga mkono chama cha upinzani, Movement for Democratic Change, MDC. Mugabe ameutaja uchaguzi wa kesho kuwa uchaguzi wa kumpinga Blair, huku wachambuzi wakisema anaitumia Uingereza kama chombo ili aweze kushinda uchaguzi huo.
Chama chake Mugabe cha ZANU-PF kimekilaumu chama kikuu cha upinzani cha Movement for Democratic Change, MDC, kwa kushirikiana na Uingereza na mataifa mengine ya kigeni. Madai haya na mbinu zinazotumiwa na chama cha rais Mugabe zimeelezewa kuwa ukiukaji wa haki za binadamu na shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu, Amnesty International lenye makao yake makuu mjini London.
Kiongozi wa chama cha MDC, Morgan Tsvangirai, amesema kampeni ya uchaguzi haimuhusu bwana Blair ndewe wala sikio, lakini inahusu kuwapa chakula raia wa Zimbabwe wanaoteseka kwa njaa, kupunguza ukosefu wa ajira na kuufufua uchumi ambao wakati wa uhuru kulikuwa na matumaini makubwa ya kunawiri.
Pasipo kujali matokeo ya uchaguzi huo, raia wameridhika na kutokuwepo na umwagikaji damu wakati wa kampeni, tofauti na hali ilivyokuwa wakati wa kampeni za chaguzi za mwaka wa 2000 na 2002, ambapo watu kadhaa waliuwawa wakati wa machafuko. Afisa mkuu wa uchaguzi nchini humo, Theophilus Gambe, amesema kuna amani na utulivu nchini kote, jambo ambalo ni la kufurahisha.
Polisi imetangaza hakuna mtu yeyote aliyeuwawa kwenye kampeni hizo huku viongozi wa upinzani wakikiri wamekuwa na uhuru wa kufanya mikutano yao na kukutana na wapigaji kura, kinyume cha yale yaliyotokea miaka mitano iliyopita ambapo chama cha MDC kililazimika kufanya kampeni za kimyakimya.
Mbunge wa upinzani amedai kuwa mmoja wa wafuasi wake alipigwa hadi akafariki dunia na vijana wanaokiunga mkono chama cha rais Mugabe, lakini polisi wamepinga wakisema kifo hicho hakikusababishwa na machafuko ya kisiasa.
Uchaguzi huo utakaoshuhudia kuchaguliwa kwa wabunge 120, utafuatiliwa kwa karibu kutathmini ikiwa Mugabe atayatimiza makubaliano yaliyoafikiwa na viongozi wa eneo hilo mwaka jana, la kuwa na uchaguzi ulio huru na wa haki.
Serikali ya Mugabe imefanya mabadiliko kadhaa ya sheria za uchaguzi, ikiwemo kutumia masanduku yanayoruhusu kura zilizotumbukizwa ndani kuonekana wazi, katika juhudi za kuzuia kura nyingi mno kutumbukizwa katika sanduku moja kwa siri. Pia vyombo vya habari vimeruhusiwa kuwa na uhuru wa kuwapa nafasi viongozi wa upinzani kutoa maoni yao.
Lakini upinzani una wasiwasi kwamba wizi wa kura huenda ukaanyika siku ya kupiga kura. Unasema pia licha ya kutokuwepo na machafuko, chama tawala cha ZANU-PF, kinaendelea kuwatisha wapiga kura, hususan katika maeneo ya mashambani, kwamba watakiona cha mtema kuni iwapo watakipigia kura chama cha upinzani cha MDC.
Chama cha MDC kiliingia katika kinyang´anyiro cha uchaguzi huo mwezi uliopita kikidai hali hazijakuwa nzuri nchini Zimbabwe za kuruhusu kuwepo uchaguzi ulio huru na wa haki. Kikasema lengo kubwa la wagombea wake kushiriki ni kuyaendeleza matumaini ya kuleta mabadiliko ya kisiasa nchini humo.