1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Je Israel inajaribu kuwahamisha Misri watu Gaza?

14 Desemba 2023

Wakati watu wengi wa Gaza wakiwa wameyakimbia makazi yao na vikosi vya Israel vikizidi kuingia kwenye eneo hilo la Palestina, kumeibuka mashaka kwamba huenda sasa raia hao wakafukuzwa kwenda nchini Misri.

Ukanda wa Gaza | Wapalestina wakipokea miili ya ndugu zao waliofariki kutoka katika Hospitali ya Martyrs ya Al-Aqsa
Jamaa wa Wapalestina waliouawa katika mashambulizi ya Israel wakiomboleza wakati walipokuwa wakichukua miili kutoka katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Al-Aqsa Martyr kwa ajili ya mazishi huko Deir al-Balah, Gaza mnamo Desemba 13, 2023.Picha: Ali Jadallah/Anadolu/picture alliance

Maafisa wa Umoja wa Mataifa na viongozi wa mataifa ya Mashariki ya Kati wameonyesha mashaka kwamba huenda sasa raia wa Gaza wakafukuzwa kwenda nchini Misri. Mazingira haya yanaibua upya historia mbaya ya kile ambacho ulimwengu wa Kiarabu unakitaja kama "Nakba" ama janga, wakirejelea yale mauaji ya kimbari ya Wapalestina wakati kulipoundwa taifa la Israel miaka 75 iliyopita. 

Israel imeapa kuliangamiza kundi la wanamgambo la Hamas ambalo maafisa wa taifa wanasema liliwaua watu wake 1,200 na wengine 240 wakiwachukua mateka. Na vita vyake tangu shambulizi hilo la oktoba 7 vimewaua zaidi ya raia 18,600 wa Gaza, hii ikiwa ni kulingana na Wizara ya Afya katika eneo linalodhibitiwa na Hamas.

Zaidi ya miezi miwili ya mapigano imepita sasa na kusababisha karibu asilimia 85 ya watu wa Gaza yenye jumla ya watu milioni 2.4 kuyakimbia makazi yao, umesema Umoja wa Mataifa, huku wengi wao wakikimbilia mji wa kusini ya mbali wa Rafah ambako tayari kumejaa pomoni.

Nini mustakabali wa watu hawa?

Mkuu wa shirika la kuwahudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa Filippo Grandi ameonya kwamba kuwalazimisha raia wa Gaza kuvuka mpaka kutaiyumbisha pakubwa Misri.

Filippo Grandi akiongea wakati wa Mkutano wa Clinton Global Initiative huko New York Hilton Midtown mnamo Septemba 18, 2023. Grandi anaonya juu ya watu wa Gaza kulazimishwa kuondoka kwenye maeneo yao. Picha: Noam Galai/Getty Images/AFP

Aliwaambia waandishi wa habari mjini Geneva kwamba ni muhimu sana kuhimiza kwamba suala la kuwahamishia raia nje ya mipaka yao halipewi kipaumbele.

Soma Pia: Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lataka usitishaji mapigano mara moja Gaza

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kwa upande wake alipokuwa huko Qatar siku ya Jumapili alionya juu ya kuongezeka kwa shinikizo la watu kukimbilia Misri Matamshi yake hayo yaliendana na ya Philippe Lazzarini, mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbiza wa Palestina, UNRWA. Yeye alionya juu ya kile kinachoshuhudiwa kuongezeka kwa watu wa Gaza wanaojaribu kukimbilia Misri kutokana na uharibifu mkubwa kaskazini mwa Gaza, huku Israel ikiwaagiza raia walioko katika mji wa kusini wa Khan Yunis kukimbilia mpakani.

Soma pia: Wajumbe wa Baraza la Usalama la UN kuzuru kivuko cha Rafah

Rais wa Mamlaka ya Palestina Mahmud Abbas, pamoja na Misri na Jordan huko nyuma waliwahi kuonya dhidi ya majaribio ya kuwalazimisha raia wa Gaza kuondoka, wakati Israel na Marekani wakiipuuzilia mbali wasiwasi huo. Msemaji wa ofisi ya Wizara ya ulinzi Israel, inayohusika na mahusiano ya raia wa Palestina alisikika akisema Israel haijawahi kuwa na wala haina mpango wa kuwahamishia raia wa Gaza huko nchini Misri. Lakini baadhi ya maafisa wa serikali ya Israel, waliunga mkono waziwazi hatua ya raia wa Gaza kuondoka tena kwa idadi kubwa.

Waziri wa masuala ya ujasusi nchini Israel Gila Gamliel alinukuliwa akisema "chaguo" la baada ya vita hivyo kumalizika huenda likawa ni kuhamasisha Wapalestina wa Gaza kuhamia kwenye makazi mapya nje ya Ukanda huo kwa hiyari kwa sababu za kibinadamu.

Sheria za kimataifa zinasemaje?

Sheria za kimataifa za binaadamu ambazo ni msingi wa Mikataba ya Geneva, inakataza kabisa kuwafukuza raia.

Pichani ni Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, au ICC, inaonekana huko The Hague, Uholanzi. ICC inazuia kuwahamisha watu kwa nguvu kwa kuwa huo ni uhalifu dhidi ya ubinaadamuPicha: Peter Dejong/AP/picture alliance

Na ikiwa hilo litafanyika kwa mustakabali wa mzozo wa kijeshi, basi ni uhalifu wa kivita, alisema Sheila Paylan, mwanasheria wa haki za kimataifa za binaadamu na mshauri wa zamani kwenye Umoja wa Mataifa.

Na chini ya sheria ya Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ICC, kuwapeleka ama kuwahamisha kinguvu idadi kubwa ya watu inaorodheshwa kama uhalifu dhidi ya ubinaadamu.

Soma pia: Ujerumani yasema amani haiwezekani Mashariki ya Kati

Abbas amesema kuwafukuza watu kutoka Gaza kutachochea kile alichokitaja "Nakba ya pili", baada ya ile ya kwanza ya mwaka 1948, ambapo Wapalestina 760,000 waliondolewa kwa lazima wakati wa vita vilivyogongana na kuanzishwa kwa taifa la Israel. Na katika vita kati ya Israel na Mataifa ya Kiarabu, vya mwaka 1967, ambapo Isreal iliudhibiti Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi pia kulikua na watu wengi walioyakimbia makazi yao.

Siku chache baada ya kuibuka vita hivyo, Rais wa Misri Abdel Fattah al-Sissi alisema watu wa Gaza wanatakiwa kusimama imara na kubaki kwenye ardhi yao.

Guterres na Waziri wa Mambo ya kigeni wa Jordan Ayman Safadi pia walizungumzia juhudi za kupangwa za Israel za kuisafisha Gaza kwa kuwafurusha raia. Hata Marekani, mshirika wa Israel haungi mkono suala hilo.

Kufuatia mazungumzo na viongozi wa eneo la Mashariki ya Kati, mwanadiplomasia wa ngazi za juu wa Marekani Antony Blinken alisema mwezi Oktoba kwamba hawaliungi mkono wazo la kuwalazimisha Wapalestina kwenda Misri.  

Soma pia:Vita kati ya Israel na Hamas katika ukanda wa Gaza ambapo mapigano hayo yamezuwia usambazaji wa misaada muhimu katika Ukanda huo

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW