Raia zaidi na waasi waondoka Ghouta Mashariki
24 Machi 2018Wizara ya Ulinzi ya Urusi imesema kiasi ya watu 105,000 wameondoka katika eneo hilo. Shirika la habari linalomilikiwa na serikali ya Syria limeripoti kuwa kiasi ya wapiganaji 7,000, familia zao pamoja na raia wanatarajiwa kuondoka leo kwenye miji ya Zamalka, Arbin na Jobar.
Kuondolewa kwa watu hao ni matokeo ya makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyofikiwa kati ya Urusi na jeshi la Syria pamoja na kundi la waasi lenye itikadi kali za Kiislamu, Faylaq al-Rahman, ambalo limekuwa likiendesha shughuli zake katika eneo hilo.
Katika taarifa yake, kundi la Faylaq al-Rahman limesema mpango huo umefikiwa ili kuruhusu wagonjwa na watu waliojeruhiwa kuondolewa mara moja kwa ajili ya kupatiwa matibabu pamoja na kuruhusu misaada kuingia katika eneo hilo ambalo limezingirwa.
Waasi kwenda kaskazini mwa Syria
Kundi hilo limeongeza kusema kuwa wapiganaji wake pamoja na ndugu zao ambao wameamua kuondoka Ghouta Mashariki watakwenda katika maeneo yanayodhibitiwa na waasi kaskazini mwa Syria, huku raia walioamua kubaki watahakikishiwa usalama wao.
Jeshi la Syria na washirika wake wa Urusi wamefanikiwa kudhibiti asilimia 90 ya Ghouta Mashariki na liko karibu kuchukua udhibiti kamili wa eneo hilo. Eneo la tatu na la mwisho ambalo bado linadhibitiwa na waasi liko katika eneo kuuzunguka mji wa Douma. Mazungumzo kwa ajili ya kuwaondoa watu kwenye mji huo bado yanaendelea.
Eneo la kwanza ndani ya mji wa Harasta lilikimbiwa na waasi siku ya Alhamisi, huku zoezi la kuwaondoa watu likianza na kuendelea hadi jana Ijumaa. Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa idadi ya watu wanaoishi Ghouta Mashariki ni 400,000.
Wengi wa watu walioondolewa leo watakwenda katika jimbo la Idlib lililoko kaskazini magharibi mwa Syria. Mabasi kadhaa yaliyowabeba watu walioondolewa Harasta yaliwasili Idlib Ijumaa usiku na awamu ya pili iliwasili leo asubuhi. Kwa mujibu wa wanaharakati wa upinzani, operesheni ya majeshi ya serikali imewaua watu 1,500 na kuwajeruhi zaidi ya 5,000.
Ama kwa upande mwingine, shirika linalofuatilia haki za binaadamu nchini Syria lenye makao yake nchini Uingereza, limesema kuwa bomu limeripuka katika jimbo la Idlib karibu na jengo la mahakama na kuwaua kiasi ya watu sita na wengine 25 wamejeruhiwa.
Wakati huo huo, ofisi ya rais wa Ufaransa imesema katika taarifa yake kwamba Rais Emmanuel Macron amezungumza kwa njia ya simu na mwenzake wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ambapo ameelezea wasiwasi wake tangu kuanza kwa operesheni inayofanywa na Uturuki dhidi ya wapiganaji wa Kikurdi katika mkoa wa Afrin. Macron amekubaliana na Erdogan kufanya mazungumzo ya kina kuhusu Syria katika siku zijazo.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFP, AP, DW https://bit.ly/2G4bTCT
Mhariri: John Juma