1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Raia zaidi ya mia moja wauliwa Kongo mnamo wiki moja

John Kanyunyu16 Machi 2022

Katika kipindi cha siku tano mfululizo, waasi kutoka Uganda ADF wamewauwa watu si chini ya mia moja katika mikoa ya Kivu ya Kaskazini pamoja na Ituri.

Demokratische Republik Kongo | Unruhen in Beni
Picha: Alexis Huguet/AFP/Getty Images

Mashambulizi hayo ya kila uchao katika mikoa wanakoendesha harakati zao magaidi wa ADF, yamekatisha tamaa mashirika ya kiraia pamoja na yale ya kutetea haki za binaadamu.

Christophe Munyanderu, mratibu wa shirika la kutetea haki za binaadamu CRDH katika wilaya ya Irumu mkoani Ituri, anasema, kwamba mauwaji yanayofanywa na ADF siku hizi, ni ishara tosha kwamba serikali ya Congo haifanyi lolote ili kuokoa maisha ya wakaazi .

Kwa upande wake Kasereka Kasayiryo, msemaji wa mashirika ya kiraia katika wilaya ya Beni anasema, kuwa inabidi majeshi ya muungano yaanzishe operesheni kabambe katika maeneo yanayoshuhudia mauwaji siku hizi kwani kutofanya hivyo kunapelekea watu kudhani kwamba hamna mpango wa kulinda raia.

"Kushuhudia upya kwa usalama mdogo katika eneo hili, hasa maeneo ambayo hayajashuhudia operesheni za pamoja kati ya jeshi la Uganda na lile la Congo inamaanisha kwamba hamna operesheni ambazo zinalenga kurudisha usalama na kuwakinga wakaazi."

Mauwaji yaendelea licha ya operesheni za pamoja

Picha: AFP via Getty Images

Na ili kutetea jeshi la muungano, msemaji wa jeshi katika eneo kubwa la Kaskazini ya mkoa wa Kivu ya Kaskazini captain Anthony Mualushayi amesema, kwamba mauwaji yanayoshuhudiwa katika wilaya ya Beni, ni ishara kwamba ADF wako mashakani

"Adui ametiwa matatani na wenzetu walioko katika operesheni za pamoja UPDF na FARDC huko Ituri, adui anaonekana kuwa na nia ya kurudi tena katika mkoa wa Kivu ya Kaskazini. Mafanikio yapo, kuna mafanikio na nadhani kwamba hapo majuzi nilitangaza matokeo ya awali ya operesheni za pamoja baina ya UPDF na FARDC."

Kwa kipindi cha siku tano mfululizo, watu sichini ya mia moja ndio wameuawa na ADF, na shambulizi la mwisho ni la jana katika kijiji cha Kisiki, kilomita  thelathini na mbili hivi, Kaskazini ya mji wa Beni.

Msimamo wa mashirika ya kiraia

Operesheni za pamoja kati ya jeshi la Congo FARDC na lile la Uganda UPDF,zilizoanzishwa mwezi  Novemba mwaka jana, zilipokelewa kwa shangwe na wakaazi wa mikoa ya Kivu ya Kaskazini pamoja na Ituri, ambako ADF anaendesha mauwaji kwani walidhani kwamba duru hii ADF atatokomezwa. La kushangaza nikuona mauwaji yanaendelea na haijulikani ni lini yatasimamishwa.

Hali hii huenda ikawapelekea wakaazi kuomba jeshi la Uganda kurudi nyumbani na kuacha FARDC jeshi la Congo kufanya kazi yake,aliiambia DW, mmoja wa viongozi wa mashirika ya kiraia aliyetaka libanwe jina lake.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW