Raila aapishwa kuwa "rais wa wananchi" Kenya
30 Januari 2018Serikali ilizima matangazo ya moja kwa moja ya vituo vitatu vikuu vya televisheni wakati kundi kubwa la watu kwa maelfu wakikusanyika katika uwanja wa Uhuru Park mjini Nairobi kuhudhuria kuapishwa kwa Odinga.
Licha ya kwamba polisi waliondolewa bila ya maelezo katika uwanja wa Uhuru Park, polisi wengi walibakia katika maeneo ya mabanda katika mji huo, ambayo ni ngome kuu ya upinzani.
Odinga alisema amejikuta katika hali ya kutokuwa na usalama wakati akihudhuria tukio hilo la kula kiapo baada ya walinzi wake kuondolewa.
Odinga mwenye umri wa miaka 73 alikula kiapo akiwa ameshika biblia huku watu wakishangiria. Kiongozi huyo wa upinzani ameiita sherehe hiyo kuwa ni hatua moja mbele kuelekea kupatikana kwa demokrasi inayofanyakazi nchini Kenya.
"Tunashuhudia kurejea kwa utawala wa kiimla, urais wa kibepari nchini mwetu na utawala wa amari, na hayo laazima yapingwe," alikiambia kituo cha utangazaji cha KTN kabla ya kuelekea kwenye hafla ya kuapishwa.
Baadae alirekebisha maelezo yake kwenye ukurasa wa twitter na kujiita "Rais wa Jamhuri ya Kenya."
National Resistance Movement marufuku
Saa kadhaa baadae serikali ikalipiga marufuku vuguvugu la taifa la upinzani, ambapo waziri w amambo ya ndani Fred Matiangi alilitangaza kuwa kundi la uhalifu.
Kwa mujibu wa sheria ya Kenya, kuwa mwanachama wa kundi la uhalifu wa kupanga inaweza kukupelekea kufungwa gerezani kwa muda usiyozidi miaka kumi, faini ya dola za Marekani zisizozidi 5,000 au vyote viwili.
Hafla hiyo ya dhihaki ilikuja baada ya miezi kadhaa ya mashaka ya kisiasa. Mahakama ya juu kabisaa nchini Kenya ilibatilisha uchaguzi wa mwezi Agosti, baada ya Odinga kudai kwamba wadukuzi wa mtandaoni waliingilia mitambo ya computer ya tume ya uchaguzi na kubadilisha matokeo kumpendelea Kenyatta.
Hukmu hiyo ndiyo ilikuwa mara ya kwanza kwa mahakama kubatilisha matokeo ya uchaguzi wa rais barani Afrika. Mahakama iliezea kasoro na ukiukaji wa sheria na kuamua dhidi ya Kenyatta kwa sababu tume ya uchaguzi ilikataa kufungua mfumo wake wa computer kutathminiwa.
Matokeo halisi ya uchaguzi
Wiki iliyopita upinzani ulitoa kile ulichokitaja kuwa matokeo sahihi yakionyesha kuwa Odinga alishinda uchaguzi wa Agosti, lakini ulikataa kusema ni kwa namna gani ulipata taarifa hizo kutoka mifumo ya computer za tume ya uchaguzi. Tume ya uchaguzi iliyataja matokeo hayo kuwa ya "bandia."
Awali polisi iliapa kuwazuwia wafuasi wa upinzani kuhudhuria sherehe ya Jumanne, na kuzusha hofu ya kutokea vurugu. Tume ya haki za binadamu inayofadhiliwa na serikali ya Kenya imesema watu wasiopungua 92 waliuawa na dazeni kadhaa wengine walishambuliwa kingono wakati wa miezi ya vurugu za uchaguzi. Wengi wao walikuwa wafuasi wa upinzani.
Watetezi w ahaki za binadamu wanautuhumu utawala wa Kenyatta kwa ukiukaji wa uhuru unaodhaminiwa na katiba, ukiwemo wa kukusanyika na kujieleza.
Mwandishi: Iddi Ssessanga/ape
Mhariri: Mohammed Abdulrahman