Raila amtaka Rais Uhuru Kenyatta kujiuzulu
8 Septemba 2017Joto la siasa linazidi kupanda nchini Kenya zikiwa zimesalia siku 39 kabla ya kufanyika uchaguzi mpya wa rais. Kinara wa upinzani Raila Odinga akizindua kampeni ya kuwaomba wafuasi wake kuchangia safari yake ya kuelekea Ikulu, ameibua mada mpya ambayo huenda ikazusha taharuki.
Odinga amesema muungano wake upo tayari kwa mkutano na tume ya kusimamia uchaguzi kwa sharti kuwa upande wa Jubilee uwepo kwenye mkutano huo wa meza ya duara, hata hivyo Odinga amesema kuwa hawajaalikwa. Mahakama ya juu ilifutilia mbali matokeo ya uchaguzi mkuu uliompa ushindi Rais Uhuru Kenyatta kwa zaidi ya kura milioni 1.4.
Tume ya uchaguzi yagawika
Wakati huo huo, tume ya kusimamia uchaguzi inafanya mkutano baada ya Mwenyekiti wake Wafula Chebukati kudai kuwa Afisa Mkuu mtendaji Ezra Chiloba alichangia kuathiri mchakato wa uchaguzi huo. Odinga amesema kuwa "Maafisa wao wa ulinzi wametolewa, baadhi yao wanapokea ujumbe unaotishia maisha yao.”
Matamshi yake yanajiri huku, tume ya kusimamia uchaguzi ikiwa imegawanyika. Barua ambayo mwenyekiti wa tume hiyo Wafula Chebukati aliandika na ikachapishwa kwenye vyombo vya habari, kuhusu masuala ambayo amemtaka Afisa mtendaji wake Ezra Chiloba ajibu, imepingwa na makamishna wanne huku wawili wakiunga.
Makamishna wanne wamekanusha kutia sahihi barua hiyo. Baadhi ya masuala ambayo Chebukati anataka Chiloba ayajibu ni pamoja na, Kwanini akaunti bandia ya barua pepe ya Chebukati ilianzishwa na kutumiwa mara elfu tisa kufungua sava ya mitambo ya IEBC?
Kwanini matokeo kwenye vituo 10366 vya kupigia kura hayakuhalalishwa? Kwanini mitambo ya tume ya kusimamia uchaguzi ilizimwa siku tatu kabla ya uchaguzi mkuu? Kwanini baadhi ya matokeo hayakusainiwa? Kwanini simu za satellite hazikufanya kazi licha ya kugharimu shilingi milioni 848? Hata hivyo wachambuzi wa masuala ya siasa sasa wanauliza, je, Chebukati hakufahamu masuala hayo kabla ya kumtangaza Kenyatta mshindi baada ya uchaguzi mkuu kufanyika.
Uhuru asisitiza atamshinda Raila
Mzozo unaotokota katika tume inayosimamia uchaguzi huenda ukaathiri imani ya wananchi kuelekea tume hiyo kabla ya uchaguzi huo wa rais. Hata hivyo kiroja cha mambo ni kwamba Chebukati kupitia wakili wake alijitetea katika mahakama ya Juu akisema kuwa uchaguzi uliendeshwa kwa njia huru na haki.
Kwa Upande wa Jubilee ukiongozwa na Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto tayari umeanza kampeini zake huku ukisema utamnyoa Odinga kama ilivyotokea tarehe nane mwezi wa nane. Hapo jana Alhamisi, kikosi hicho kilikita kambi katika ngome yake ya Bonde la ufa.
Kenyatta alisema" Wakenya ni wale wale, wembe ni ule ule, sisi hatuna shida, tutarudi kwa wakenya tukiongozwa na Mungu, kuwaomba kura tarehe 17, na tuhakikisha kuwa mzee huyo tumpeleke nyumbani asirudi kusumbua Ruto mwaka 2022”. Kwa sasa Makamishna wa tume ya kusimamia uchaguzi wanafanya mkutano kulainisha masuala yenye utata kwenye tume hiyo yanayotishia kuigawanya tume hiyo.
Mwandishi: Shisia Wasilwa
Mhariri: Saumu Yusuf