1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Raila kupinga matokeo ya uchaguzi mahakamani

Shisia Wasilwa16 Agosti 2017

Kiongozi wa upinzani Kenya, Raila Odinga, asema upinzani hautakubali haki za Wakenya kukandamizwa na kwamba wataonyesha jinsi uchaguzi ulivyochakachuliwa. Upinzani utafungua kesi kupinga matokeo ya uchaguzi.

Kenia PK Raila Odinga zur Wahlniederlage
Picha: Reuters/T. Mukoya

J3.16.08.2017-Kenia: Interview - MP3-Stereo

This browser does not support the audio element.

Siku nane baada ya uchaguzi mkuu kufanyika nchini Kenya, Muungano mkuu wa upinzani nchini Kenya - NASA, umetoa taarifa yake kwa vyombo vya habari leo. Muungano huo tangu mwanzo ukishikilia kuwa uchaguzi huo hukuwa huru, haki na wazi. Tume ya kusimamia uchaguzi ingali inasubiri kupokea fomu za uchaguzi juma moja baada ya uchaguzi mkuu kumalizika.

Muungano mkuu wa upinzani unadai kuwa tume hiyo imechelewesha kuwakabidhi karatasi hizo kwa sababu inazichakachua ili zionekane kuwa sambamba na matokeo iliyotangaza kuwa Rais Kenyatta alimshinda Odinga kwa kura milioni 1.4. Muungano huo ukikataa kumtambua Kenyatta kuwa rais mteule. Odinga amesema kuwa hawatakubali matokeo hayo hadi tume ya kusimamia uchaguzi iyajibu maswala ambayo wameyaibua.

NASA imeelezea kuwa wangekubali uhalali wa matokeo hayo iwapo wangepatiwa fomu za uchaguzi za kuonesha kuwa matokeo yale ni sawa na yale yaliyotangazwa na tume ya kusimamia uchaguzi. Tume hiyo bado haijatoa fomu 34A elfu 10 za uchaguzi huo kwa umma. Odinga aliyeonekana mtulivu amewasuta wote ambao wamekuwa wakitaka akubali ushinde wakiwemo waangalizi wa kimataifa.

UN yasema uchaguzi ulikuwa wa huru na haki

Muungano huo wa upinzani sasa unadai kuwa serikali inaharamisha na kuyatisha mashirika ya kutetea haki za binadamu nchini ili kuyazuaia kuwasilisha kesi mahakamani kupinga matokeo ya uchaguzi mkuu uliokamilika hivi majuzi. Mashirika hayo yanadai kuwa mchakato mzima wa uchaguzi huo ulikosa uwazi na haki. Maafisa wa polisi walivamia shirika la uongozi bora la AFRICOG leo asubuhi, japo lengo la uvamizi wake halifahamiki. Hata hivyo, serikali imeyapa mashirika hayo siku tisini kutimiza masharti ya kisheria.

Picha: picture-alliance/AP Photo/S. A. Azim

Wakati huo huo, Umoja wa Mataifa umesema kuwa uchaguzi huu uliendeshwa kwa njia huru na haki na kusema kuwa rais Kenyatta alimshinda Odinga. Ombi la Odinga la kutaka Umoja huo kutathmini matokeo ya uchaguzi wa tarehe nane, lilikataliwa. Matamshi kama hayo yakitolewa na Rais wa Marekani Donald Trump aliyewataka Wakenya kudumisha amani utulivu na kusuluhisha utata wao mahakamani.

Uamuzi huo umeafikiwa na kikao cha muungano huu kilichojumuisha vinara wake, wataalamu wa kifundi, wataalamu wa masuala ya sheria, katiba na uongozi pamoja na viongozi wa kada mbali mbali wa muungano huo.

Hata hivyo muungano wa NASA haukutoa ushahidi uliokuwa nao kwa wanahabari kwa hofu ya kumwaga mtama mbele ya kuku wengi. Tamko la leo la Odinga ni nafuu kwa Wakenya wengi ambao walidhani kuwa angeitisha maandamano. Yeyote anayepanga kupinga matokeo ya urais ana hadi siku ya Ijumaa kufanya hivyo kwa mujibu wa katiba. Macho yote sasa yanaelekezwa katika idara ya mahakama kuona jinsi itakavyoamua. Mwaka 2013, Mahakama ya Juu ilitupilia mbali kesi iliyowasilishwa na upinzani kupinga matokeo ya urais ambapo Uhuru Kenyatta alitangazwa mshindi.

Mwandishi: Shisia Wassilwa, DW, Nairobi

Mhariri: Mohammed Khelef

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW