Raila Odinga akubali kugawa fedha za vyama vya NASA
27 Julai 2021Mzozo huo wa kugawa hela za vyama vya siasa vya upinzani umekuwa ukiendelea kwa miaka 4 sasa. Kwenye waraka maalum, kiongozi wa chama cha upinzani cha Orange Democratic Movement, ODM, Raila Odinga aliweka bayana kuwa hela za hazina ya vyama vya siasa zitagawanywa kwa vyama vilivyounda muungano wa NASA ambao sasa unaregarega. Duru zinaeleza kuwa waraka huo uliwasilishwa pia kwa kiongozi wa chama cha Amani National Congress, ANC,Musalia Mudavadi, Moses Wetangula wa Ford-Kenya na Isaac Ruto wa Chama cha Mashinani.Kwenye kikao na waandishi wa habari, Kiongozi wa chama cha upinzani cha Wiper, Kalonzo Musyoka aliipokea vizuri hatua hiyo na kuelezea kuwa hawawezi kushindwa kufikia mwafaka.
''Chama cha ODM sasa kinaridhia kugawanya fedha za hazina za vyama vya siasa.Hizi ni fedha zilizokusanywa pamoja. Nilijuwa wapo wenye misimamo mikali ndani ya ODM wanaompotosha Raila. Tulikaa na kuzungumzia maswala haya tu ya fedha za vyama vya siasa.'', alisema Kalonzo.
''Sisi kama chama tuna mikakati ya kutosha''
Hata hivyo haijakuwa bayana iwapo Raila Odinga na Kalonzo Musyoka sasa wamefikia makubaliano rasmi ya kisiasa ya pamoja.Kwa mtazamo wake Kalonzo Musyoka wa chama cha Wiper anashikilia kuwa watafanya kazi kisiasa na yule atakayekuwa na mtazamo kama wao katika uchaguzi mkuu ujao wa 2022.Saa chache zilizopita uongozi wa Wiper ulitangaza rasmi kuuanza mchakato wa kujiondoa kwenye muungano wa upinzani wa NASA na kujiandaa kupanga mikakati na muungano mpya wa Okoa Kenya-OKA.Wiki iliyopita kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi alitangaza pia kuwa wamefikia uamuzi kama huo.
''Sisi kama chama tuna mikakati ya kutosha, kwa sababu ya kuchukuwa uongozi wa serikali kwenye uchaguzi unaokuja wa mwaka 2022.''
Kongamano la chama cha ODM
Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna alithibitisha mwanzoni mwa wiki hii kuwa viongozi hao wamekuwa wakifanya majadiliano ya moja kwa moja.Yote haya yanajiri wakati ambapo chama cha upinzani cha ODM kinajiandaa kufanya kikao cha baraza lake kuu siku ya Alhamisi ili kujadili mipango ya uchaguzi mkuu ujao pamoja na atakayewawakilisha.Kwa sasa Raila Odinga anaizuru kaunti ya Murang'a katika kile kinachoonekana kuwa juhudi za kuwavutia wapiga kura wa eneo la kati la Kenya. Kwengineko wanasiasa wa eneo la Mlima Kenya wako mbioni kuunda chama chao na kujiweka katika nafasi muhimu kabla ya uchaguzi mkuu.