Raila Odinga atafakari hatua za kuchukua baada ya uchaguzi
14 Agosti 2017Raila Odinga mwenye umri wa miaka 72 anasisitiza ndiye mshindi katika uchaguzi huo na ametoa mwito kwa wafuasi wake kutokwenda kazini hii leo ili kuomboleza vifo vya wale waliouawa katika maandamano kupinga kutangazwa Rais Uhuru Kenyatta kuwa mshindi wa nafasi ya urais huku wafuasi wa kiongozi huyo wa upinzani wakiendelea kusubiri tamko aliloahidi atalitoa kesho Jumanne kuhusiana na hatua za baadaye watakazochukua.
Hata hivyo baada ya karibu kipindi cha wiki moja ambapo shughuli zilisimama nchini humo hali imeonekana kurejea katika hali ya kawaida katika jiji la Nairobi hii leo huku wengi wakionekana kurejea kazini na kutokubali kuendelea kupoteza muda kwa kusalia majumbani mwao licha ya kiongozi wa upinzani kuwataka kufanya hivyo.
Mmoja wa wafanyabiashara ya matunda katika jiji la Nairobi, Alex Kilonzo, alisikika akisema kuwa iwapo angekuwa ana pesa basi angeligoma lakini kawa sasa hawezi kufanya hivyo.
Hii ni mara ya nne kwa Raila Odinga ambaye ni mwanasiasa wa upinzani kushindwa katika uchaguzi huo na amekuwa akiendelea kusisitiza kuwa alishinda katika chaguzi za mwaka 2007 na pia mwaka 2013.
Baada ya tume ya uchaguzi kutangaza matokeo ya mshindi wa kiti cha Rais Ijumaa iliyopita maandamano ya watu wenye hasira yalifanyika Ijumaa usiku na Jumamosi katika maeneo ambayo ni ngome kuu ya Odinga na pia katika eneo la mabanda jijini Nairobi ambapo watu 16 waliuawa akiwemo msichana mwenye umri wa miaka 9.
Vyombo vya usalama Kenya vyakanusha kuuawa watu wasio na hatia
Polisi nchini Kenya wamekanusha kuuawa kwa waandamanaji wasio na hatia wakidai waliouwa ni watu waliokuwa na silaha na walionekana kuwashambulia maafisa wa polisi na waliofanya vitendo vingine vya uhalifu kama vile ubakaji pamoja na wizi.
Kenya mara kadhaa imekuwa ikikabiliwa na mzozo wa uchaguzi ikiwa ni pamoja na mwaka 2007 wakati Odinga aliposhindwa katika uchaguzi wa mwaka huo ambao waangalizi wengi walikiri ulikuwa na mapungufu ikiwa ni pamoja na ukiukwaji wa taratibu za uchaguzi.
Uchaguzi wa mwaka huu umeibua kumbukumbu ya vurugu zilizotokea baada ya uchaguzi uliofanyika muongo mmoja uliopita ambapo watu 1,100 waliuawa huku wengine 600,000 wakilazimika kuyahama makazi yao.
Historia inaonesha kuwa marais watatu kati ya wanne nchini Kenya wanatoka katika kabila la wakikuyu huku mmoja akiwa ni mkalenjini hali inayoonesha kuyatenga makabila mengine makubwa nchini humo kama wajaluo kushika madaraka ya urais katika kipindi cha nusu karne sasa.
Wakati hayo yakiendelea wafuasi wa mgombea wa kiongozi wa upinzani Raila Odinga kutoka kabila la kijaluo hapo jana Jumapili katika eneo la mabanda la mathare jijini Nairobi walipambana na wafuasi wa kundi la wakikuyu wanaomuunga mkono Uhuru Kenyatta. Hata hivyo Japeth Koome afisa wa polis katika jiji la Nairobi alikanusha kuwepo tukio hilo katika eneo la Mathare.
Licha ya vurugu kuonekana kutulia wafuasi wa Raila Odinga bado wanasubiri tamko kutoka kwa kiongozi huyo huku Odinga mwenyewe akisema hajakata tamaa na amewataka kusubiri tamko atakalolitoa hapo kesho Jumanne.
Umoja wa Mataifa, Uingereza, Ufaransa na Umoja wa Ulaya wamemtaka Odinga kufuata taratibu za kisheria katika kutafuta kile anachodai. Katibu Mkuu wazamani wa Umoja wa Mataifa Koffi Annan ambaye alishiriki katika kutanzua mzozo ulioibuka baada ya uchaguzi wa mwaka 2007/2008 amewaonya viongozi wa kisiasa nchini Kenya kuwa waangalifu na kauli zao wanazotoa kipindi hiki.
Mwandishi: Isaac Gamba/afpe/ape
Mhariri: Mohammed Khelef