Raila Odinga ataka "Punguza Mizigo" ikataliwe
2 Septemba 2019Raila amesema kuwa muasisi wa mswada huo anajitakia makuu na kuongeza kuwa mikakati ya kuleta mwafaka nchini maarufu BBI itashughulikia mabadiliko kwenye serikali na kisha baadaye kupigiwa kura ya maoni.
Iwapo, matukio ya siasa yanayoendelea nchini Kenya yatasalia jinsi yalivyo basi ni bayana kuwa mazingira ya uchaguzi mkuu ujao yameanza kujengwa, huku wanasiasa wakiunda miungano kwa misingi ya kuirekebisha katiba. Wachambuzi wa masuala ya siasa wakisema kuwa kipute hicho kitakuwa kati ya Raila Odinga na naibu rais William Ruto.
Kwenye kile kinachoonekana kuwa ni kuusuta mswada wa Punguza Mzigo, unaopigiwa upatu na kiongozi wa chama cha Thirdway Alliance Ekuru Aukot, kiongozi wa upinzani ambaye sasa anaonekana kukosa makali ya kuikosoa serikali, Raila Odinga anaomba mabunge kutupilia mbalia mswada huo. Hata hivyo Raila hajatangaza nia ya kuwania kiti hicho akinukuliwa kusema kuwa atafanya hivyo wakati mwafaka utakapojiri.
Aipongeza Kaunti ya Siaya kuwa ya kwanza kuukataa mswada huo
Raila amepongeza kaunti ya Siaya kwa kuwa bunge la kwanza nchini Kenya kuukata mswada huo ambao unajadiliwa katika mabunge yote kote nchini humo. Ameyataka mabunge yote katika kaunti ya Nyanza ambayo ni ngome ya upinzani kuukataa. Kwingineko naibu rais William Ruto aliendelea kwenda kinyume na matakwa ya bosi wake Uhuru Kenyatta ambaye mara nyingi amewataka wafuasi wake kuacha kupiga siasa na badala yake kuwahudumia wananchi. Ruto ametaja mikakati ya kuleta mwafaka maarufu BBI iliyoanzishwa na Raila na Rais Kenyatta kuwa itakayochochea ukabila.
Wanaoupigia debe mkakati wa BBI wanapendekeza kubuniwa kwa nafasi ya waziri Mkuu, manaibu wake wawili, rais pamoja na naibu wake. Ruto alimkosoa Raila kwa kusema kuwa tatizo lake ni kuwa mara nyingi akishindwa huwa hakubali.
Zaidi ya wabunge 20 wa mlima Kenya walihudhuria hafla hiyo katika kaunti ya Kirinyaga iliyopuuzwa na Gavana Ann Waguru ambaye hivi karibuni amemuunga mkono Raila. Waiguru alinukuliwa akisema kuwa Mlima Kenya kwa sasa uko tayari kwa uongozi wa Raila Odinga kauli inayoonekana kuligawanya eneo hilo ambalo limetoa marais watatu katika historia ya Kenya.