Raila Odinga kupepea bendera ya NASA
27 Aprili 2017Muungano wa Upinzani nchini Kenya NASA umemtangaza Raila Odinga kuwa mgombea wake wa urais katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Tarehe 8 Agosti huku Kalonzo Musyoka akitangazwa kuwa mgombea mwenza.Raila Odinga atachuana katika uchaguzi huo mkuu na rais aliyeko madarakani Uhuru Kenyatta. Katika sherehe zilizofanyika katika uwanja wa Uhuru Park Alhamisi viongozi watano wa muungano huo wa Nasa walishirikiana bega kwa bega kuzungumzia Umoja na mshikamano wa chama hicho kitakachochuana na chama cha Jubilee kinachoongozwa na Uhuru Kenyatta na William Ruto.
Wakenya watapiga kura kuwachagua Rais , wabunge na viongozi wengine katika uchaguzi huo unaotarajiwa kuwa na mchuano mkali kati ya muungano wa NASA ukiongozwa na Raila Odinga na chama cha Jubilee kikiongozwa na Uhuru Kenyatta.Kutangazwa kwa Raila Odinga kushikilia bendera hiyo ya muungano wa NASA katika uchaguzi wa rais ni hatua iliyokuwa ikisubiriwa kwa hamu kubwa na pande zote za kisiasa hasa kutokana na mivutano iliyokuwa ikiendelea katika muungano huo juu ya nani hasa anastahili kuipeperusha bendera hiyo.
Hata hivyo kwa upande mwingine haikuwa tangazo la kushtuwa kwa kuwa tayari huko nyuma duru kutoka ndani ya Muungano huo zilikuwa zimeshadokeza kwamba atakayeiongoza NASA katika uchaguzi wa rais ni 'Agwambo''Raila Amolo Odinga ambaye ni kiongozi wa chama cha Orange Democratic Movement ODM mojawapo ya vyama vitano vinavyounda muungano huo mkuu wa upinzani NASA.
Viongozi wa NASA waliojitokeza kuzungumza katika sherehe za kumtangaza mgombea wao wa urais walisikika wakizungumza kwa mbwembwe nyingi na kutamba kwamba huu ni mwaka wa kuikomboa kwa mara nyingine Kenya waliodai imetawaliwa kwa misingi ya uwongo na mabavu bila ya kufuatwa Sera.Gavana wa Mombasa Hassan Joho alitangaza katika mkutano huo kwamba yeye ni adui mkubwa wa Uhuru Kenyatta na William Ruto viongozi wa chama cha Jubilee kutokana na sera zao za kuikandamiza kaunti yake ya Mombasa na wananchi wa pwani wa ujumla.Mchuano wa urais Agosti 8 utaamua kwa mara nyingine juu ya hatma na historia ya Kenya.
Mwandishi: Saumu Mwasimba/Reuters
Mhariri: Daniel Gakuba