Raila Odinga: NASA kugeuka Vuguvugu la Ukombozi
25 Oktoba 2017Raila Odinga ameweza kuwahutubia wafuasi wa upinzani katika bustani ya Uhuru mjini Nairobi, licha ya mkutano huo kupigwa marufuku na Kaunti ya Jiji la Nairobi leo Jumatano, kwa hoja kwamba ulikuwa kinyume cha sheria.
Pindi alipopanda jukwaani Raila Odinga ameweka bayana kuwa muungano wa NASA sasa umekuwa vuguvugu la kisiasa kwa ajili ya ukombozi, akiongeza kuwa hawatatulia wakati udikteta unakithiri.
''Kesho hatuendi kupiga kura, na baada ya keho, tarehe 27 Oktoba, mambo yatakuwa tofauti'', amesema Odinga.
Raila Odinga aliyejiondoa kwenye kinyang'anyiro amekuwa akiwahimiza wafuasi wake kuandamana ili kuishinikiza tume ya uchaguzi na mipaka, IEBC kufanya mageuzi.
IEBC yatuhumiwa kuegemea upande mmoja
Anailaumu tume ya uchaguzi ya IEBC kwa kuegemea upande mmoja kwa kushindwa kuyatimiza matakwa yao ya mageuzi jambo wanalodai linauongeza uwezekano wa uchaguzi wa kesho kugubikwa na wizi wa kura. Raila anasisitiza kuwa mambo yatageuka kuanzia kesho Alhamisi.
Kwa upande mwengine Uhuru Kenyatta anayewania urais tena kwa tiketi ya Jubilee amesema uchaguzi utaendelea kesho Alhamisi kama ilivyopangwa.
Yote hayo yakindelea baadhi ya wapiga kura wamekuwa wakijitahidi kuelekea vijijini kuweza kupiga kura katika maeneo ya bunge walikosajiliwa.Mamia ya wafuasi wa Jubilee kutokea kaunti ya Muranga walimiminika vituoni kupata usafiri wa bure uliofadhiliwa na uongozi wa kaunti. Viyuo vua kupigia kura vinatarajiwa kufunguliwa mwendo wa saa kumi na mbili kamili kesho asubuhi.
Vyombo vya usalama kukaa chinjo
Kaimu Waziri wa usalama wa taifa Dr Fred Matiang'i ameweka bayana kuwa mipango usalama imekamilika. Awamu hii maafisa wa usalama watajikita katika kuhakikisha wapiga kura wanalindwa ili wasivamiwe na wanaopinga uchaguzi mpya wa rais kufanyika.
''Tutahakikisha vituo ofisi zote 290 za majimbo ya uchaguzi zinapatiwa ulinzi wa kutosha'', amesema Matiang'i.
Dr Matiangi anasisitiza kuwa maafisa wa tume ya uchaguzi IEBC nao pia watapewa ulinzi kamili hasa katika maeneo wanakohofia vurugu.
Majina ya wagombea wote 8 walioshiriki kwenye uchaguzi wa tarehe 8 mwezi Agosti mwaka huu yapo kwenye orodha na makaratasi mapya ya kupigia kura. Japheth Kavinga Kaliyu ni mmoja wa wagombea hao wa binafsi na amefurahi kuwa Kenya ina nafasi ya kusogea mbele.
Mahakama ya juu iliubatilisha uchaguzi wa rais wa Agosti 8 kwasababu ya makosa na dosari zilizojitokeza.
Mwandishi: Thelma Mwadzaya
Mhariri: Gakuba Daniel