1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Ahmadinejad akutana na mwenzake wa Lebanon

Kabogo Grace Patricia13 Oktoba 2010

Viongozi hao wawili wamekutana mjini Beirut, baada ya Rais Ahmadinejad kuanza ziara yake rasmi nchini Lebanon, ikiwa ni ya kwanza kuifanya nchini humo tangu aingie madarakani.

Rais wa Iran Mahmoud Ahmadinejad (Shoto), akisalimiana na mwenzake wa Lebanon, Michel Suleiman, baada ya kuwasili katika Ikulu ya Lebanon.Picha: AP

Rais Mahmoud Ahmadinejad wa Iran leo amekutana na mwenzake wa Lebanon, Michel Suleiman baada ya kuwasili mjini Beirut kwa ziara yake rasmi ya kiserikali ya siku mbili. Hii ni ziara ya kwanza ya kiongozi huyo nchini Lebanon tangu alipoingia madarakani, mwaka 2005.

Baada ya kuwasili kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Beirut, Rais Ahmadinejad alilakiwa na Spika wa Bunge Nabih Berri. Ujumbe wa kundi la Hezbollah pia ulikuwepo katika uwanja huo wa ndege kwa ajili ya kukutana na kiongozi huyo wa Iran. Maelfu ya wafuasi kutoka kundi la Kishia nchini Lebanon la Hezbollah linaloungwa mkono na Iran pamoja na Wairan wanaoishi Lebanon, walijipanga katika mitaa mbalimbali kuelekea uwanja wa ndege kwa ajili ya kumsalimu Rais Ahmadinejad.

Akiwa ndani ya gari la wazi, kiongozi huyo wa Iran aliupungia mkono umati mkubwa wa watu ambao walikuwa wakirusha mchele na maua waridi. Viongozi wa Hezbollah walionekana wakiwa wamevalia nguo za kiraia huku wakiendesha magari meusi aina ya Jeep kwa ajili kudhibiti mistari ya wananchi waliokuwa wamejipanga kuelekea kwenye uwanja wa ndege katika kuonyesha kwamba walikuwa wakihusika na masuala ya usalama.

Kabla ya kuanza mazungumzo yake na Rais Suleiman, Rais Ahmadinejad aliyeongozana na Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje, Manoucher Mottaki na ujumbe wa wafanyabiashara alipokelewa na Waziri Mkuu wa Lebanon Saad Hariri katika Ikulu ya nchi hiyo ya Baabda. Kiongozi huyo wa Iran pia anatarajiwa kuhudhuria mkutano wa kundi la Hezbollah mjini Beirut ambapo atapanda jukwaani pamoja na kiongozi wa kundi hilo, Sayyed Hassan Nasrallah ambaye tangu mwaka 2006 amekuwa akionekana katika mikutano na mikutano ya waandishi habari kwa njia ya video kutokana na sababu za kiusalama.

Maeneo mengine atakayotembelea

Kesho kiongozi huyo wa Iran atatembelea eneo la kusini mwa Lebanon na maeneo ya karibu na mpaka na Israel na kuhutubia katika kijiji cha Bint Jbeil, ambacho kiliteketezwa wakati wa vita vya mwaka 2006 kati ya Israel na Hezbollah. Ziara hiyo ya Rais Ahmadinejad ina lengo la kukuza na kuimarisha uhusiano wa kisiasa na kiuchumi kati ya nchi hizo mbili pamoja na kujadiliana kuhusu masuala ya kimataifa na ya kikanda.

Hata hivyo, wachambuzi mjini Beirut wanasema kuwa ziara hiyo ya Ahmadinejad nchini Lebanon ni kwa ajili ya kuonyesha kuliunga mkono kundi la Hezbollah na kuishambulia Israel. Ziara ya kiongozi huyo imewakasirisha baadhi ya viongozi wa Lebanon ambao wanazipinga sera za Hezbollah ambalo ni kundi kubwa la upinzani kwa baraza la mawaziri linaloongozwa na Waziri Mkuu Saad Hariri na ambalo linaungwa mkono na mataifa ya Magharibi. Samir Geagea kiongozi wa kisiasa ambaye ni Mkristo na anayejulikana kwa kuupinga msimamo wa Hezbollah, amesema Rais Ahmadinejad angepokelewa vizuri nchini Lebanon iwapo angefanya ziara hiyo akiwa kama rais wa Iran na sio rais wa baadhi ya maeneo ya Lebanon.

Kiongozi huyo wa Iran ambaye alikuwa amalize ziara yake ya siku mbili hapo kesho, sasa ataikamilisha siku ya Ijumaa ambapo atakutana na Waziri Mkuu wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, anayetarajiwa kuizuru Lebanon siku hiyo kwa ajili ya mkutano kati ya Lebanon, Iran na Uturuki utakaofanyika mjini Beirut.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (DPAE)

Mhariri:Abdul-Rahman