Rais Ahmedinejad atembelea Kusini mwa Lebanon
14 Oktoba 2010Ziara hii inamfanya Rais Mahmoud Ahmedinejad asimame kilomita nne tu kutoka taifa la Israel, ambalo yeye binafsi halitambui na amewahi kulifananisha na "saratani ya ubongo" ambayo lazima ing'olewe, ikiwa nchi za Mashariki ya Kati zinataka kubakia salama. Hili ni jambo ambalo Waisrael wengi hawachukui.
Erfrat, kijana wa Kiyahudi ambaye amekuwa akiishi kwenye mji wa Metulla ulio Kaskazini ya Israel kwa mwaka mmoja sasa, anasema yeye na marafiki zake wanaichukulia ziara hii ya kiongozi wa Jamhuri ya Kiislam ya Iran mlangoni pa Israel kwa hali ya tahadhari, japo sio kwa uadui mkubwa.
"Labda ni jambo linaloliza kengele ya tahadhari sana kufikiria kwamba Ahmedinejad yupo karibu yetu sana, hapa Metulla." Anasema Erfrat.
Tayari vyombo vya habari vya Israel vinairipoti ziara hii ya Ahmedinejad kama ni dalili ya kiongozi huyo wa Iran kuonesha ushawishi wake ulivyo mkubwa kwa jirani yao ambaye wamepigana naye mara kadhaa, Lebanon. Na wengine wamefika umbali wa kuiita ziara hii kama uchokozi wa wazi, ambao unakusudiwa kuionesha Israel kwamba imeshindwa kuivunja taswira ya Iran nchini Lebanon, ambayo ina wafuasi wengi wa madhehebu ya Shia.
Rais Ahmedinejad mwenyewe leo hii (14 Oktoba 2010) alikutana na mwenyeji wake, Rais Michel Sleiman, na kuisifu Lebanon kwa mapambano yake dhidi ya utawala wa Kizayuni huku akiahidi kwamba Iran itaendelea kuiunga mkono Lebanon muda wote na kwa vyovyote hadi dola hiyo ya Kiyahudi itoweke.
Ni kauli kama hii, ambayo inapendelewa pia na kutumiwa na kiongozi wa wanamgambo wa Hizbullah, Hassan Nasrallah, ambayo Israel na washirika wake wa nchi za Magharibi, ikiwemo Marekani, wanaichukulia kama ni uhafidhina wa kutupwa wa serikali ya Iran, ambao lazima upigwe vita.
Tayari Israel imesema kwamba kwa kumkaribisha kwake Ahmedinejad, Lebanon inajiweka katika lile kundi la nchi zinazotambuliwa kama "mhimili wa uovu" duniani.
Lakini hali ilivyo nchini Lebanon kwenyewe ni tafauti. Rais Ahmedinejad amepokelewa kama shujaa na waungaji mkono wake, hasa katika jamii ya Kishia, ambao wengi ni wafuasi wa kundi la Hizbullah lililopigana kiume na Israel mwaka 2006. Vita hivyo vya mwezi mmoja, vinaelezewa na wachambuzi wa Mashariki ya Kati kama vita vya mwanzo kumalizika na kuiacha dola ya Kiyahudi ikiwa imeshindwa.
Ushindi wa kundi la Hizbullah unanasibishwa moja kwa moja na msaada wa hali na mali kutoka Iran, ambayo haifichi mtazamo wake kuhusiana na Israel.
Nchini Israel kwenyewe, ziara hii itaendelea kuzua mijadala kila pahala. Uadui uliopo baina yake na majirani zake wa Kiarabu, kwa upande mmoja, na urafiki uliopo baina ya Iran na majirani hao kwa upande mwengine, ni jambo ambalo haliipi raha Israel.
Erfrat anasema kwamba eneo lote la Metulla lina hisia mchanganyiko kuhusiana na ziara hii.
"Kuna aina fulani ya hisia, ama nyengine kali sana au nyengine ndogo sana: ni mchanganyiko wa hasira kidogo na woga kidogo, ni aina ya hisia za kutokuwa na uhakika wa jambo, lakini sio zaidi ya hapo."
Mwandishi: Mohammed Khelef/ZPR/AFPE
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman