Rais Ali Bongo apelekwa Morocco kwa matibabu
30 Novemba 2018Rais wa Gabon Ali Bongo aliwasili nchini Morocco jana jioni, kuendelea na matibabu baada ya kuugua mwezi mzima nchini Saudi Arabia, akisumbuliwa na maradhi ambayo hayajaelezwa rasmi.
Duru za kidiplomasia zimesema kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 59 ataendelea kupona na kupata afueni katika hospitali nchini humo, kulingana na maelekezo ya madaktari.
Hakuna picha zozote zilizoonyesha kuwasili kwake, hali inayozidisha wasiwasi nchini Gabon, kuhusu afya ya rais huyo.
Kukosekana kwa taarifa za kutosha, na usiri uliogubika kifo cha rais wa zamani Omar Bongo, ambaye ni baba yake rais wa sasa, kumesababisha uvumi wa kila aina, ukiwemo kwamba Ali Bongo amepooza, au hata amekwishaaga dunia.
Katika juhudi zakuondoa uvumi huo, ofisi ya rais ilikubali mapema mwezi huu kwamba rais huyo alikuwa mgonjwa mahututi, na kusisitiza alikuwa akiendelea kupata nafuu.