Rais aliyeondolewa madarakani nchini Peru awekwa kizuizini
9 Desemba 2022Hapo jana Alhamisi, siku moja baada ya kuondolewa madarakani, Castillo alikuwa chini ya kizuizi cha muda na kisha baadaye alifikishwa mbele ya Mahakama ya Juu ya nchi hiyo kwa njia ya video.
Waendesha mashtaka walifanya upekuzi mkali kwenye ofisi za rais na baadhi ya majengo ya wizara kutafuta ushahidi dhidi ya Castillo, anayechunguzwa kwa kile kinatajwa kuwa "uasi na njama chafu" dhidi ya taasisi za dola.
Mwanasiasa huyo wa mrengo wa shoto alipandishwa kizimbani kwa muda mfupi na waendesha mashtaka walimwomba Jaji atoe idhini kwa vyombo vya dola kuendelea kumshikilia kwa muda wa wiki moja.
Jaji anayesikiliza kesi hiyo aliridhia ombi hilo la waendesha mashtaka licha ya hoja za wakili wa Castillo aliyesema "hakuna kosa la uasi lililotendwa" na mwanasiasa huyo.
Castillo mwenyewe aliketi kimya akionekana kuwa mwenye wasiwasi na alijibu maswali machache mahakamani kuhusiana na mipango yake ya kulivunja bunge na kutawala kwa amri badala ya katiba.
Tangazo lililomwangamiza Castillo na wadhifa wake wa urais
Tangazo la Castillo mnamo siku ya Jumatano la kutaka kulivunja bunge kwa lengo la kumaliza mzozo wa kisiasa na kiuchumi unaolikabili taifa hilo la America ya Kusini ndiyo lilikuwa chanzo cha kuondolewa kwake madarakani.
Muda mchache baada ya kulihutubia taifa, wabunge walikutana na kupiga kura ya kumvua wadhifa wake na kisha kumwapisha aliyekuwa makamu wa rais Dina Boluarte, kuchukua hatamu za dola.
Hapo jana rais wa Mexico Andres Manuel Lopez Obrador alifichua taarifa kuwa Castillo aliomba hifadhi ya kisiasa baada ya kuvuliwa madaraka lakini kiongozi huyo alikamatwa kabla ya kuondoka nchini Peru.
Wizara ya mambo ya kigeni ya Mexico imesema hivi sasa inafanya mashauriano na wenzao wa Peru kuona uwezakano wa kumpatia Castillo hifadhi ya kisiasa.
Mrithi wa Castillo akabiliwa na shinikizo la kuipatia nchi utulivu
Wakati hayo yakijiri rais mpya wa Peru Dina Boluarte ameanza kazi chini ya shinikizo kubwa ikiwemo kutoka kwa wafuasi wa rais aliyetimuliwa madarakani.
Maelfu ya wafuasi wa Castillo waliteremka mitaani hapo jana kwenye mji mkuu Lima na miji mingine ikiwemo Ayacucho na Puno kulaani kuondolewa kwa mwanasiasa huyo madarakani na kutaka aachiwe huru.
Wengine wametoa miito ya kuitishwa kwa uchaguzi mpya bila kuchelewa. Miongoni mwa hao ni Antonia Medina amabye amesema "Niko hapa kwa ajili ya uchaguzi mpya. Kama rais Castillo anaondoka, basi kila mtu lazima aondoke. Tuitishe uchaguzi, kwa sababu rais anachaguliwa kwa kura za walio wengi"
Msukosuko huo wa kisiasa unaoiandama Peru ni mwendelezo wa mivutano ndani ya mkaundi ya kisiasa ya nchi hiyo ambayo kura za kuwaondoa marais madarakani limegeuka jambo la kawaida.
Marekani imeisifu nchi hiyo kwa kusimamia "uthabiti wa kidemokrasia" huku Umoja wa Ulaya umeelezea uungaji wake mkono kwa njia zilizochukuliwa na taasisi za nchi hiyo katika kushughulikia kadhia inayoendelea.