1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Ashraf Ghani aikimbia Afghanistan

15 Agosti 2021

Rais wa Afghanistan Ashraf Ghani ameikimbia nchi yake leo Jumapili baada ya wanamgambo wa Taliban kuuzingira mji mkuu, Kabul. 

Washington | Präsident Ashraf Ghani
Rais Ashraf Ghani wa AfghanistanPicha: Alex Brandon/AP/picture alliance

Maafisa wawili wa serikali ambao hawakutaka majina yao kutajwa wameliambia shirika la habari la Associated Press kuwa Ghani ameondoka Afghanistan na inaarifiwa amekimbilia taifa jirani la Tajikistan. 

Mkuu wa Baraza la Maridhiano ya Taifa nchini Afghanistan Abdullah Abdullah pia amethibitisha habari hizo kupitia mkanda wa video.

Kuondoka kwa Ghani kunatoa taswira halisi ya uwezekano wa kundi la Taliban kuchukua madaraka nchini Afghanistan wakati wowote kuanzia sasa.

Wapiganaji wa kundi hilo waliingia kwenye viunga vya pembezoni mwa mji mkuu wa Kabul leo Alfajiri baada ya kupata mafanikio makubwa katika siku za karibuni kwa kuikamata miji mingi nchini humo.

Taliban yaamuru wapiganaji wake kutoingia katikati ya mji 

Wanamgambo wa Taliban waliingia mji mkuu, Kabul siku ya JumapiliPicha: Jalil Ahmad/REUTERS

Ripoti zinasema wapiganaji wa Taliban wameamriwa kusalia kwenye viunga vya pembezoni mwa mji huu huku serikali mjini Kabul ikiarifu kuwa inajiandaa "kukabidhi madaraka"

Wapiganaji wa Taliban wameuzingira mji wa Kabul kufuatia mafanikio makubwa waliyoyapata dhidi ya vikosi vya serikali ambavyo vimedhihirisha kwamba havina uwezo wa kuilinda nchi hiyo bila msaada wa jeshi la Marekani.

Iwapo Taliban itaukamata mji mkuu Kabul itashuhudiwa kundi hilo linaloegemea misimamo mikali ya kidini likirejea madarakani baada ya miongo miwili tangu lilipoondolewa mamlakani na vikosi vya Marekani kufuatia mashambulizi ya Septemba 11.

"Taliban inaviamuru vikosi vyake vyote kubakia kwenye maeneo ya pembezezoni mwa Kabul, na kutojaribu kuingia kwenye mji huo" ameandika msemaji wa Taliban kupitia ukurasa wake wa Twitter baada ya wakaazi wa Kabul kuripoti kwamba wamewaona wapiganaji wa kundi hilo kwenye viunga vya mji.

Msemaji huyo amesema hadi mipango ya kukabidhi madaraka itakapokamilika usalama wa mji huo mkuu uko chini ya vikosi vya serikali.

Rais Ghani kutangaza kujiuzulu na kukabidhi madaraka?

Rais wa Afghanistan, Ashraf GhaniPicha: Rahmatullah Alizadah/Xinhua News Agency/picture alliance

Kabla ya kuondoka nchini mwake rais Ghani -- aliyetarajiwa kujiuzulu wakati wowote -- alitangaza kukubali kushindwa, na katika ujumbe alioutoa kwa njia ya video amewatolea wito wanajeshi waliosalia kuimarisha hali ya usalama.

Kuna wasiwasi wa kutokea ombwe la ulinzi kwenye mji huo mkuu katika wakati maelfu wa polisi na askari wa vikosi vingine wamekimbia vituo vyao vya kazi na kutelekeza sare pamoja na silaha.

"Ni wajibu wetu na tutautimiza kwa njia yoyote inayowezekana" alisema Ghani, saa chache baada ya Taliban kuchukua udhibiti wa magereza mawili na kuwafungulia maelfu ya wafungwa.

Serikali iliashiria mapema leo kwamba mashauriano yameanza kuepusha umwagikaji wa damu mjini Kabul na kukabidhi madaraka kwa Taliban.

"Raia wa Afghanistan hawapaswi kuwa na shaka ... hakutakuwa na mashambulizi kwenye mji mkuu na madaraka yatakabidhiwa kwa serikali ya mpito" amesema waziri wa mambo ya ndani Abdul Sattar Mirzakwal katika ujumbe kwa njia ya video.

Hofu imetanda wakati mataifa ya magharibi yakihamisha raia wake

Ubalozi wa Ujerumani nchini AfghanistanPicha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Uwezekano wa Taliban kutwaa madaraka umezusha wasiwasi mkubwa miongoni mwa waakazi wa mji wa Kabul wanaohofia misimamo mikali ya kiislamu inayohubiriwa na wanamgambo hao.

Wakati hayo yakijiri mataifa ya magharibi yameendelea na juhudi zake za kuwaondoa wafanyakazi wake.

Rais Joe Biden wa Marekani ameamuru kutumwa kwa wanajeshi 1,000 wa ziada kusaidia kuondolewa kwa wafanyakazi wa ubalozi na maelfu ya Waafghani waliofanya kazi pamoja na vikosi vya Marekani.

Kwa upande wake Ujerumani imetangaza kufungwa kwa ubalozi wake mjini Kabul. Mataifa mengine ikiwemo Uingereza yanazidisha nguvu ya kuwahamisha raia wake kutoka Afghanistan.