Rais Bashir amemfuta kazi waziri wa mambo ya nchi za nje
20 Aprili 2018Rais wa Sudan Omar Hassan al Bashir amemfuta kazi waziri wa mambo ya nchi za kigeni wa nchi hiyo Ibrahim Ghandour. Shirika la habari la serikali SUNA limeripoti kwamba waziri huyo alitimuliwa baada ya kusema wanadiplomasia wa Sudan katika mataifa ya kigeni hawajalipwa mishahara kwa miezi kadhaa.
Katika hotuba yake kwa wabunge hapo jana Ghandour, aliyeongoza mazungumzo ya kuondolewa vikwazo vya muongo mmoja vilivyowekwa na Marekani mnamo Oktoba mwaka uliopita, alisema wizara yake pia ilikuwa imeshindwa kulipa kodi kwa balozi kadhaa za Sudan kwa sababu ya mapungufu ya fedha serikalini.
Sudan imekabiliwa na matatizo ya fedha huku ikikabiliwa na uhaba mkubwa wa fedha za kigeni ambao umesababisha uchumi wa taifa hilo la Afrika Mashariki kuendelea kudorora.