1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Biden aanza ziara Mashariki ya Kati

Daniel Gakuba
13 Julai 2022

Rais Joe Biden wa Marekani anaanza leo ziara ya siku nne Mashariki ya Kati itakayomfikisha Israel na Saudi Arabia. Miongoni mwa mengine, ziara hiyo ina malengo ya kujaribu kuanzisha uhusiano baina ya nchi hizo mbili.

US-Präsident Joe Biden
Picha: Susan Walsh/AP/dpa/picture alliance

Kituo cha kwanza cha ziara hiyo ya Rais Joe Biden kitakuwa nchini Israel, ambako atafanya mazungumzo na viongozi wa taifa hilo ambao wanaendeleza juhudi za kujenga mshikamano dhidi ya Iran, na baadaye ataitembelea mamlaka ya ndani ya Wapalestina, ambayo viongozi wake wanachukizwa na msimamo wa Marekani wa kushindwa kuizuia Israel kuendeleza unyanyasaji katika maeneo ya Wapalestina inayoyakalia kimabavu.

Mzozo kati ya Israel na Wapalestina sio suala geni kwa Biden, ambaye kwa mara ya kwanza aliuzuru ukanda huo mwaka 1973 wakati huo akiwa seneta.

Kushawishi uhusiano baina ya Israel na Saudia

Mshauri wa Rais Biden juu ya masuala ya usalama wa taifa, Jake Sullivan, amesema wakati wa ziara ya kiongozi huyo wa Marekani mashariki ya kati, uhusiano baina ya Israel na majirani zake wa kikanda utapewa kipaumbele.

Mjini Jerusalem bendera za Marekani na Israel zinapepea pamoja katika maandalizi ya kumpokea Rais Joe BidenPicha: Tania Kraemer/DW

''Ni matumaini na matarajio yetu kuwa mnamo siku za usoni Israel itajumuishwa kikamilifu kikanda, na kwa hali ya kipekee itakuwa na uhusiano mwema na Saudi Arabia,''  amesema Sullivan na kuongeza kuwa ''ingawa kazi kubwa itakafanyika wakati wa ziara hii hatua yoyote ya kujenga uhusiano kati ya nchi hizo itakuwa mchakato mrefu.'' 

''Hata hivyo tunatarajia maendeleo katika mwelekeo huo, na bila shaka ni suala la msingi tunapoanza ziara kuelekea mashariki ya kati.'' Amesema mshauri huyo wa Biden.

Iran imesema mapema leo kuwa juhudi hizo za Marekani zitaambulia patupu, ikiwa zinanuia kuitafutia usalama Israel.

Mvutano baina ya Iran na Israel

Mara tu baada ya kuwasili Israel ataonyeshwa mfumo mpya wa ulinzi wa anga wa Israel, ambao jeshi la nchi hiyo linaunadi kuwa wenye uwezo wa kupambana na mashambulizi ya ndege za Iran zisizoendeshwa na rubani.

Ndege zisizo na rubani za Iran zinaikosesha usingizi IsraelPicha: Iranian Army Office/ZUMA/IMAGO

Israel imeapa kufanya chochote kinachowezekana kuhujumu mipango ya Iran kuunda silaha za nyuklia, na inapinga vikali mazungumzo ya kufufua makubaliano ya kimataifa juu ya mpango wa nyuklia wa Iran.

Rais Biden anatarajiwa kuwasili nchini Saudi Arabia kesho kutwa Ijumaa, na ziara hiyo inaangaziwa sana baada ya rais huyo kutoa kauli ya kuitaja Saudi Arabia kuwa taifa linalopaswa kutengwa, kufuatia mauaji ya mwandishi wa habari mkosoaji wa ufalme wa Saudi Arabia, Jamal Khashoggi.

Huko Saudi Arabia, Biden anajaribu kutafuta utangamano katika soko la mafuta ya petroli, baada ya bei ya bidhaa hiyo kupanda sana kufuatia kuanza kwa vita vya Ukraine.

 

Vyanzo: AFPE,APE

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW