1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Joe Biden adai kuiacha Marekani ikiwa salama zaidi

14 Januari 2025

Rais Biden: Trump atairithi Marekani yenye washirika imara,wenye maadui dhaifu.

Hotuba ya Joe Biden,wizara ya mambo ya nje ya Marekani
Rais Joe Biden akihutubia kuhusu sera zake za njePicha: Roberto Schmidt/AFP

Rais Joe Biden ameisifu sera yake ya nje, akisema imeiacha Marekani mahala salama. Katika hotuba yake  Jumatatu iliyoangazia zaidi sera yake ya nje, alisema nchi hiyo iko katika hali thabiti ya kiuchumi kutokana na uongozi wake na kwamba rais ajaye Donald Trump atarithi taifa imara kabisa.

Biden amelihutubia taifa wakati rais Mteule Donald Trump akiwa anajiandaa kuapishwa madarakani Januari 20. Amesifia sera zake za nje kwa kusema, Marekani hivi sasa ni salama na rais ajae atakabidhiwa nchi ikiwa imara na yenye kuaminika zaidi kuliko ilivyokuwa miaka minne iliyopita:
 

Rais Joe Biden akizungumza katika wizara ya mambo ya nje wa MarekaniPicha: Roberto Schmidt/AFP

"Ni wazi kwamba utawala wangu unaikabidhi nchi kwa utawala ujao ikiwa imara. Na tunawaachia Marekani ikiwa na marafiki zaidi na washirika imara ambao maadui zao ni dhaifu na wanaokabiliwa na shinikizo. Marekani ambayo kwa mara nyingine inaongoza,inayaleta pamoja mataifa, na kuweka ajenda, pamoja na kuwashawishi wengine kuwa nyuma ya mipango na mitazamo yetu''

Rais huyo anayemaliza muda wake madarakani ameusifu utawala wake kwa kazi iliyoufanya katika kuitanuwa Jumuiya ya kijeshi ya NATO pamoja na kuwakusanya washirika wake kuisadia Ukraine kwa msaada wa kijeshi na kupambana na Urusi lakini pia kuimarisha Marekani kiviwanda na kuwa katika nafasi nzuri ya kushindana na China.

Soma pia: Je, utawala mpya wa Trump utawaridhisha Wamarekani wenye asili ya kiarabu?Katika hotuba aliyoitowa katika wizara ya mambo ya nje , amejisifia kwamba kutokana na uongozi wake hivi sasa Marekani inapata mafanikio katika ushindani wa kilimwengu ikilinganishwa na miaka minne iliyopita huku akidai kwamba nchi hiyo haikuingia vitani kufanikisha yote hayo. Na juu ya hilo amezungumzia pia kuhusu vita vya Mashariki ya Kati:

"Kuhusu vita kati ya Israel na Hamas ,tuko ukingoni hatimae kufikia makubaliano yanayohusiana na pendekezo tulilolitowa miezi kadhaa iliyopita. Nimejifunza kwa miaka mingi niliyotumikia umma kutokata tamaaa kabisa.''

Mtoto mchanga aliyekufa kwa baridi kali GazaPicha: Omar Ashtawy/ZUMAPRESS.com/picture alliance

Rais Joe Biden kutoka chama cha Demokratic ambaye ameiongoza Marekani kwa muhula mmoja tu,aliingia madarakani wakati ulimwengu ukishuhudia janga kubwa kabisa ambalo halijawahi kutokea katika kipindi cha karne moja,na mipango yake ya kurekebisha mahusiano na washirika wa Marekani, ilisabishwa na mahusiano mabaya iliyokuwepo kwa miaka minne ya uongozi wa Trump, aliyeingia kwa sera yake ya kutanguliza Marekani kwanza.

Biden pia alikuwa na kipindi kigumu kilichoshuhudia mparaganyiko katika mpango wake wa kuondoka Afghanistan, vita vya Urusi nchini Ukraine na mashambulizi ya Hamas Oktoba 7 dhidi ya Israel, yaliyozusha vita vikubwa Mashariki ya Kati.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW