1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Biden katika ziara ya siku mbili nchini Angola

3 Desemba 2024

Rais wa Marekani Joe Biden yuko nchini Angola katika ziara yake ya kwanza na ya pekee kama Rais wa Marekani katika eneo la Kusini mwa Afrika. Ziara ya Biden inaangazia mradi mkubwa wa ujenzi wa reli.

Joe Biden Kap Verde
Picha: Ben Curtis/dpa/picture alliance

Rais Joe Biden aliwasili katika katika jiji la Luanda, Jumatatu jioni kwa ziara ya siku mbili inayotarajiwa kujikita kwenye mradi wa kimataifa wa kukarabati miundombinu ya reli inayotumiwa kusafirisha madini kutoka nchi za bara hadi kwenye bandari ya Lobito nchini Angola kwa ajili ya kuuza nje ya nchi.

Kutokana na safari ya rais wa Marekani nchini Angola, serikali ya nchi hiyo imetangaza hii leo Jumanne Desemba 3 na kesho Jumatano Desemba 4 kuwa ni siku za mapumziko huku kukiwa na ulinzi mkali katika mji mkuu wa Luanda, jiji lililo na wakaazi takriban milioni 9.5.

Kushoto: Rais wa Angola Joao Lorenco. Kulia: Rais wa Marekani Joe BidenPicha: Luis Tato/Andrew Caballero-Reynolds/AFP

Biden atafanya mazungumzo hii leo na Rais wa Angola Joao Lourenco na Rais wa Zambia Hakainde Hichilema katika mji mkuu Luanda na baadaye anatarajiwa kutoa hotuba katika Jumba la kitaifa la Makumbusho ya Utumwa. Biden anatarajiwa pia kutangaza ahadi za ziada kwa mradi huo na vile vile kwa ajili ya sekta ya afya, maswala ya hali ya hewa na mipango ya nishati safi. 

Soma Pia: Angola yaongoza mkutano wa kufufua juhudi za amani DRC 

hapo kesho Jumatano Rais wa Marekani Joe Biden, atakwenda Lobito, mji wa bandari ulio umbali wa takriban kilomita 500 kusini mwa mji mkuu Luanda.

Bandari ya Lobito ndiyo kitovu cha mradi wa Ukanda wa Lobito ambao umepata mikopo kutoka Marekani, Umoja wa Ulaya na wadau wengine kwa ajili ya kuikarabati reli muhimu inayounganisha nchi za bara zenye utajiri wa madini za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Zambia ambazo zinashirikiana na mradi huo wa Ukanda wa Lobito kusafirisha madini kwenda nje ya nchi.

Rais wa Zambia Hakainde HichilemaPicha: picture alliance/dpa/AP

Mshauri wa maswala ya usalama katika ikulu ya Marekani John Kirby amenukuuliwa na waandishi wa Habari akisema haya ni mabadiliko Chanya katika ushirikiano wa Marekani bara la Afrika. Amesema utawala wa Rais Joe Biden unaoondoka madarakani una matumaini makubwa kwamba wakati uongozi mpya utakapoingia mwakani utaliangalia hili na kuiona thamani yake, kwa mtazamo kwamba uhusiano huu utasaidia kuliendesha bara la Afrika kuwa salama zaidi, lenye ustawi mkubwa na utulivu wa uhakika wa kiuchumi.

Soma Pia: Angola: Mashambulizi ya serikali dhidi ya demokrasia yanafikia kiwango cha kutisha 

Maafisa wawili waliohudumu katika utawala uliopita wa Donald Trump wamesema ingawa ingawa ziara ya Biden nchini Angola inafanyika katika siku za mwisho za urais wake, wanaamini kwamba Donald Trump atakaporejea madarakani mnamo mwezi Januari mwakani anaweza kuuunga mkono mradi huo wa ujenzi wa reli na kuendelea kuwa mshirika wa karibu wa Angola.

Chanzo: AFP

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW