Rais Bush ziarani Georgia
10 Mei 2005Tbilisi:
Rais George W. Bush wa Marekani amesema leo mjini Tbilis kuwa mapinduzi ya amani ya Jamhuri ya zamani ya Urussi, Georgia ya mwaka wa juzi ni mfano mzuri wa kuigwa na nchi nyingine zinazopigania demokrasia. Urussi itanufaika zaidi kuwa na nchi za kidemokrasia katika mipaka yake. Rais Bush akiwahutubia Wandishi wa Habari mbele ya mwenyeji wake, Mikhail Saakashvili, amesema kuwa mapinduzi ya waridi yana nguvu kihistoria kwa sababu hayakuwatia moyo Wageorgia peke yao isipokuwa watu wengine pia duniani. Rais Bush ameongeza kusema kuwa wakati unapokuwa na nchi za amani katika mipaka yako ndivyo ambavyo utaweza kunufaika. Ana matumaini kuwa Urussi itatambua manufaa ya kuwa na nchi za kidemokrasia katika mipaka yake. Rais Bush ni Kiongozi wa kwanza wa Marekani kulitembelea eneo la Caucasus ambalo kwa muda mrefu limekuwa chini ya ushawishi wa Urussi.