Rais Bush ziarani Ulaya
21 Februari 2005Brussels:
Rais wa Marekani, George W. Bush, ambaye yuko Brussels, Ubelegiji leo atatoa mwito wa kuanzishwa upya uhusiano uliopo kati ya Marekani na nchi za Ulaya. Atatoa mwito huo baada ya kile anachokieleza kuwa hali iliyotokea kuhusu vita dhidi ya Irak na atawaomba Washirika wake waungane zaidi katika masuala mengine kama vile kuzihusu Iran, Siria na mwenendo wa amani ya Mashariki ya Kati. Rais Bush, kwa mujibu wa hotuba yake iliyosambazwa kabla, atasema kuwa kumalizika kwa mgogoro wa Waisraeli na Wapalestina ni lengo kubwa la Marekani na nchi za Ulaya. Atausifu pia Umoja wa Ulaya. Atawakumbusha pia Wamarekani na wakazi wa Ulaya kuwa ushirikiano uliopo kati yao ni muhimu sana kwa ajili ya usalama wao na amani. Rais Bush leo, atakutana na Rais Jacque Chirac wa Ufaransa na Waziri Mkuu wa Ubelegiji, Guy Verhofstadt, wakosoaji wakubwa wa vita vya Irak. Atakutana na Kansela Gerhard Schröder wa Ujerumani siku ya Jumatano mjini Mainz.