1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Idadi kubwa ya maseneti wapiga kura ya kumwondoa madarakani

Sylvia Mwehozi12 Mei 2016

Baraza la maseneti nchini Brazil limeidhinisha kura ya kumfungulia mashitaka rais Dilma Roussef ambapo sasa atapaswa kumuachia madaraka makamu wake ili mchakato wa kushitakiwa uendelee.

Brasilien Dilma Rousseff
Picha: Reuters/U. Marcelino

Baraza la maseneti nchini Brazil limeidhinisha kura ya kumfungulia mashitaka rais Dilma Roussef ambapo sasa atapaswa kumuachia madaraka makamu wake ili mchakato wa kushitakiwa uendelee.

Rais Dilma Roussef atakabidhi madaraka kwa hasimu wake , makamu wa rais Michel Timer baada ya idadi kubwa ya maseneta kujitokeza kumpigia kura ya kuidhinisha rais huyo kushitakiwa katika mchakato ambao uliendelea usiku kucha wa kuamkia siku ya alhamis.

Idadi kubwa ya wajumbe katika baraza lenye maseneta 81 ndiyo iliyohitajika katika kupititisha maamuzi hayo ya kusimamisha kazi kwa miezi sita wakati mchakato wa mashitaka ukiendelea. Makamu wa rais Temer atashika wadhifa huo unaohitimisha miaka 13 ya utawala wa chama cha wafanyakazi cha mrengo wa kushoto cha rais Roussef. Temer amesema anaandaa serikali yake itakayojaribu kunusuru uchumi wa nchi hiyo uliodorora.

Baraza la seneti la nchini BrazilPicha: Getty Images/I. Estrela

Ikiwa imebaki miezi mitatu kabla ya kuanza kwa mashindano ya Olympic mjini Rio de Janaiero, Brazil sasa inapambana kustawisha uchumi ulioporomoka pamoja na kushughulikia kashfa za rushwa zilizokita mizizi kwa wanasiasa na wafanyabiashara.

Awali mahakama ya juu nchini humo imeamuru kufanyike uchunguzi wa tuhuma za rushwa dhidi ya kiongozi wa upinzani seneta Aecio Neves ambaye alikuwa mpinzani wa Bi. Roussef katika uchaguzi wa mwaka 2014. Anatuhumiwa kwa utakatishaji wa fedha na kuchukua hongo, ni miongoni mwa maseneta ambao wanaunga mkono suala la kumshitaki rais.

Migogoro mingi iliyopo kwa sasa imeigawa nchi hiyo, wapo ambao wanataka rais ashitakiwe, wengine bado wanaona kwamba chama hicho kilichoko madarakani kimefanya kazi kubwa ya kuwaondolea umaskini mamilioni ya raia.

Jitihada za rais huyo kuepukana na kikaango cha kuondolewa madarakani , zilififia siku ya jumatano baada mahakama kukataa ombi la mwanasheria mkuu la kubatilisha mchakato huo.

Waandamanaji mjini Brasilia nchini BrazilPicha: Reuters/P. Whitaker

Seneta Paulo Paim, mshirika wa rais Roussef anaona kuwa hakuna "muujiza" na kwamba wanapambana kushinda. Magno malta , seneta kutoka chama cha upinzani cha PR anasema kura hiyo ni sindano inayohitajika katika kuiponya nchi.

Hata hivyo wapo wanaodhani kuwa hata kama Roussef ataondolewa, matumaini ni madogo ya kupata maendeleo. Mmoja wa wananchi anayeunga mkono kura hiyo Sulineide Rodrigues anasema kuwa na hapa namnukuu "hatufikirii kwamba Temer atakuwa mzuri, ingawa "tutaendelea kuwaondoa hadi hapo atakapopatikana yule anayewasikiliza wabrazil" mwisho wa kunukuu.

Wakati kikao cha maseneta kikiendelea, kumekuwa na mapambano ya pande mbili katika miji ya Brasilia na Rio.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman