Rais Donald Trump azindua Bodi ya Amani mjini Davos
22 Januari 2026
Bodi hiyo itaratibu juhudi za usitishwaji wa vita vya Israel katika Ukanda wa Gaza, lakini pia ujenzi mpya wa eneo hilo la Kipalestina. Kwenye uzinduzi, Trump amesifu uanzishwaji wa chombo hicho na kusema sio cha watu wa Marekani, bali ni cha ulimwengu mzima.
Wengi wana wasiwasi kwamba ni chombo kinachokuja kutoa upinzani kwa Umoja wa Mataifa ambao umekuwa na jukumu la suala zima la amani ya ulimwengu. Kulingana na Trump kwenye uzinduzi huo, kila mmoja anatamani kuwa sehemu ya Bodi hiyo, licha ya kwamba washirika wengi wa Marekani wamechagua kutojiunga. "Donald Trump: Rais wa Marekani: "Kama sehemu ya kumbukumbu ya kihistoria ya mipango mikubwa ya amani, leo tunatangaza maelezo zaidi kuhusu Bodi ya Amani. Bodi hii inaweza kuwa moja ya vyombo muhimu zaidi kuwahi kuundwa, na ni heshima kubwa kwangu kuwa mwenyekiti wake. Tulipata wazo, kisha tukaanzisha na wakaniomba niwe Mwenyekiti. Niliona heshima sana waliponiomba nifanye hivyo. Tuna watu wengi na vijana wazuri sana wanaoiongoza. Inaendeshwa vizuri -- tayari imeanza. Na, kila nchi -- karibu kila nchi inataka kuwa sehemu ya bodi hii." Amesema Trump.
Kundi la viongozi na maafisa waandamizi kutoka mataifa 19 ikiwa ni pamoja na washirika wake kutoka Argentina na Hungary waliungana na Trump mapema leo katika shughuli ya kurekodi majina yao kwenye hati ya kuanzishwa kwa bodi hiyo ambayo amesema imejaa viongozi mchanganyiko, mashuhuri sana na wa kawaida.
Hati ya Bodi hiyo ambayo lengo la awali lilikuwa ni kuratibu mpango wa amani wa Gaza baada ya vita kati ya Hamas na Israel, hata hivyo inaonyesha kuwa na majukumu mapana zaidi ya kusuluhisha mizozo ya kimataifa, na kuibua wasiwasi kwamba Trump anataka kupambana na Umoja wa Mataifa. Hata hivyo, Trump mwenyewe alisema Bodi hiyo itafanya kazi "kwa kushirikiana" na Umoja wa Mataifa.
Na suala jingine ambalo linaonekana kuzua utata ni hatua ya Trump kumwalika Rais wa Urusi Vladimir Putin, aliyevamia Ukraine miaka minne iliyopita. Na tayari amesema Putin amekubali kujiunga.
Ili kuwa mwanachama wa kudumu, unatakiwa kulipa mchango wa dola bilioni moja. Hili nalo limeobua ukosoaji mkubwa kwamba bodi hiyo huenda ikaja kuwa chombo cha nchi wanachama kulipia ili nazo zinufaike.
Uingereza na Ufaransa, washirika wakubwa wa Marekani ni miongoni mwa waliojitenga na bodi hiyo. Wameeleza mashaka yao, na Uingereza ilisema haitashiriki hata hiyo hafla ya uzinduzi.
Washirika wakubwa wa Trump, Waziri Mkuu wa Hungary, Victor Orban na Rais wa Argentina Javier Milei walikuwa sambamba na Trump kwenye shughuli ya kusaini. Aidha maafisa kutoka Bahrain, Morocco, Armenia, Azerbaijan, Bulgaria, Indonesia, Jordan, Kazakhstan, Kosovo, Pakistan, Paraguay, Paraguay, Qatar, Saudi Arabia, Uturuki, Umoja wa Falme za Kiarabu, Uzbekistan na Mongolia pia walisaini hati hiyo na Trump.
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, anayesakwa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu kutokana na vita vyake huko Gaza pia amekubali kujiunga na bodi hiyo ingawa hakuwa kwenye hafla ya kutia saini. Kwa ujumla nchi 30 imethibitisha kujiunga, kati ya 50 zilizoalikwa, imesema Ikulu ya White House.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio alisema kwenye hafla hiyo kwamba lengo la kwanza la bodi hiyo ni kuhakikisha kwamba makubaliano ya amani katika Ukanda wa Gaza yanakuwa ya kudumu.
Trump hata hivyo amesema Hamas wanapaswa kusalimisha silaha kama ilivyo kwenye makubaliano ya amani, vinginevyo utakuwa ndio mwisho wa kundi hilo.