Trump akwaruzana tena na Zelensky
24 Aprili 2025
Trump aidha amemshutumu Zelensky kwa kukataa kutambua udhibiti wa Urusi kwenye jimbo la Crimea.
Mjini Washington, Rais Donald Trump wa Marekani amesema anaamini amefikia makubaliano na marais wote wawili wa Ukraine Volodymyr Zelensky na Vladimir Putin wa Urusi ya kuvimaliza vita vnavyoendelea nchini Ukraine.
Hata hivyo amekiri alipozungumza na waandishi wa habari katika ikulu ya White House kwamba, imekuwa ngumu sana kwake kuzungumza na Zelensky, tofauti na alivyotarajia.
Maafisa wengine wa Marekani walisema mapema Jumatano kwamba bado hakujafikiwa makubaliano na Marekani inaweza kujiondoa kwenye mazungumzo ya amani ikiwa hakutapigwa hatua za haraka, Baadae Trump alisema akiwa kwenye ofisi yake ya Oval kwamba anadhani Urusi iko tayari na wamefikia makubaliano, lakini bado hawajakubaliana na Zelensky.
Soma pia: JD Vance azitaka Urusi na Ukraine kufikia makubaliano
Alisema "Kila kitu kiko sawa. Ninachotaka mimi ni kuona vita vinamalizika. Sitojali kama wote watafurahia, ama pande zote zimekubaliana. Siupendelei upande wowote. Siaki kupendelea upande wowote. Ninataka kuona kunafikiwa makubaliano. Ninataka kuokoa maisha ya watu."
Na alipoulizwa kuhusiana na pendekezo la Marekani kwa Ukraine la kuitambua haki ya Urusi kuimiliki Rasi ya Crimea, Trump hakutaka kulizungumzia moja kwa moja, bali aliendelea tu kusisitiza haipendelei ama Urusi au Ukraine, bali anachokitaka ni vita kumalizika. Crimea ni eneo linalotambulika kimataifa kuwa ni sehemu ya Ukraine na Kyiv inasema inaitaka rasi hiyo ya Bahari Nyeusi. Urusi ililichukua eneo hilo mwaka 2014.
Kwa ujumla matamshi ya Trump yakatofautiana na yale yaliyotolewa awali na maafisa wa ngazi za juu kwenye serikali yake. Masaa machache kabla ya kuzungumza na waandishi hao wa habari, msemaji wa White House Karoline Leavitt aliwaambia waandishi wa habari kwamba Trump amechoshwa na kasi ya mazungumzo na kwamba Zelensky anaonekana kuchukua mwelekeo mbaya.
Soma pia:Kremlin: Mazungumzo na Kiev yatafanyika vikwazo vikiondolewa
Zelensyk akatisha ziara yake Afrika Kusini kufuatia mashambulizi ya Urusi
Mjini Johannesburg Rais Zelensky amesema analazimika kukatisha ziara yake nchini Afrika Kusini na kurejea nyumbani baada ya Urusi kuishambulia Kyiv usiku wa kuamkia Alhamisi.
Zelensky aliwasili Jumatano usiku nchini humo kwa ziara ya kikazi, katikati ya tuhuma hizi mpya za Trump kwamba kiongozi huyo alikuwa akiviendeleza vita kutokana na kukataa kutambua haki ya Urusi kulimiliki eneo hilo la Crimea, kipengele ambacho ni muhimu kwenye makubaliano ya amani.
Lakini akiwa safarini, Urusi imefanya mashambulizi makubwa ya droni na makombora mjini Kyiv usiku wa kuamkia leo na kuwaua watu 9 na kuwajeruhi wengine zaidi ya 60, miongoni mwao watoto 6, hii ikiwa ni kulingana na mamlaka za Ukraine.
Soma pia:Vikosi vya Urusi vyashambulia Odesa kwa droni
Vikosi vya uokozi na dharura vimesema mashambulizi hayo yalisababisha moto kuwaka kwenye maeneo karibu 40 na vipande vya vyuma vilianguka na kuharibu magari. Mji wa Kharkiv ambao ni wa pili kwa ukubwa nchini Ukraine, nao ulishambuliwa, amesema meya ya mji huo.
Wakati haya yakiendelea, kutoka mjini Washington taarifa zinasema Katibu Mkuu wa NATO Mark Rutte anakwenda mjini humo hii leo kuzungumza na maafisa waandamizi wa serikali ya Marekani, miongoni mwao ni Waziri wa Mambo ya Nje Marco Rubio na Mshauri wa Usalama wa Taifa Mike Waltz, na mazungumzo yao yatajikita kwenye juhudi za kuvimaliza vita nchini Ukraine, hii ikiwa ni kulingana na NATO na Wizara ya mambo ya Nje ya Marekani.