1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Emmerson Mnangagwa atangazwa mshindi wa Urais Zimbabwe

Angela Mdungu
27 Agosti 2023

Tume ya taifa ya uchaguzi nchini Zimbabwe imemtangaza Rais Emmerson Mnangagwa kuwa mshindi wa kiti cha Urais katika uchaguzi uliofanyika Jumatano 23.08.2023.

Wafuasi wa ZANU-PF wakishangilia katika mkutano wa kampeni
Wafuasi wa ZANU-PF wakishangilia katika mkutano wa kampeniPicha: Philimon Bulawayo/REUTERS

Hata hivyo upinzani umeyakataa matokeo ya uchaguzi ambao waangalizi wa kimataifa walisema pia kuwa haukukidhi viwango vya demokrasia.

Kulingana na matokeo rasmi yaliyotangazwa na mwenyekiti wa Tume ya taifa ya uchaguzi ya nchi hiyo Justice Chigumba, Rais Emmerson Mnangagwa mwenye miaka 80, ameshinda kwa kupata asilimia 52.6 ya kura dhidi ya asilimia 44 za mpinzani wake mkuu Nelson Chamisa, mwenye miaka 45.

Katika uchaguzi huo, raia wa Zimbabwe walikwenda katika vituo vya kupigia kura kuchagua rais na  wabunge Jumatano na Alhamisi, katika zoezi lililotawaliwa na ucheleweshaji kitendo ambacho kilichochea shutuma za udanganyifu na ukandamizaji wa wapigakura zilizotolewa na upinzani.

Matokeo ya uchaguzi wa Rais yalipokelewa kwa nderemo bna wafuasi wachache wa chama tawala katika ukumbi wa mikutano, lakini msemaji wa chama cha "Citizens Coalition for Change" cha Nelson Chamisa alisema kuwa chama hicho hakikutia sahihi majumuisho ya mwisho aliyoyataja kuwa ya "uongo". Alisema kuwa hawawezi kuyakubali matokeo na kwamba hivi karibuni chama hicho kitatangaza hatua inayofuata.

Akijibu madai ya upinzani, Rais Mnangagwa amesema wanaohoji matokeo ya uchaguzi wanapaswa kwenda  mahakamani.

Rais Emmerson MnangagwaPicha: Iranian Presidency/AA/picture alliance

Uchaguzi wa Zimbabwe ulikuwa ukitazamwa katika mataifa ya Kusini mwa Afrika kama kipimo cha uungwaji mkono wa chama cha Mnangagwa cha ZANU-PF ambacho utawala wake wa miaka 43 umekuwa ukikabiliwa na mdororo wa uchumi na tuhuma za uongozi wa kibabe.

Waangalizi wa uchaguzi waainisha dosari zilizojitokeza

Ijumaa, waangalizi wa kigeni wa uchaguzi walisema kuwa zoezi hilo halikuendana na viwango vya kikanda na kimataifa.

Ujumbe wa waangalizi kutoka Jumuiya ya Ulaya, Jumuiya ya Madola na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) uliorodhesha masuala kadhaa yaliyotiliwa shaka yakiwemo kupigwa marufuku kwa mikutano ya vyama vya upinzani, dosari katika orodha ya wapiga kura, upendeleo wa vyombo vya habari vya taifa katika kuripoti matukio na vitisho kwa wapiga kura.

Soma zaidi: SADC: Uchaguzi Zimbabwe haujakidhi mahitaji ya katiba

Rais Emmerson Mnangagwa aliyetangazwa mshindi katika uchaguzi huo wa Jumatano aliingia madarakani katika muhula wake wa kwanza mwaka 2017 baada ya mapinduzi yaliyomuondoa madarakani hayati rais Robert Mugabe.

Kiongozi mkuu wa upinzani nchini Zimbabwe Nelson ChamisaPicha: Tsvangirayi Mukwazhi/AP Photo/picture alliance

Mwaka mmoja baadaye, alimshinda kwa tofauti ndogo Nelson Chamisa kwa mara ya kwanza katika uchaguzi ambao viongozi wa upinzani waliulaani kuwa ulikuwa na vitendo vya udanganyifu.

Uchaguzi wa wiki hii, ulilazimika kuingia katika siku ya pili kwa sababu ya kucheleweshwa kwa karatasi za kupigia kura katika baadhi ya maeneo muhimu ikiwemo Harare, ambapo ni ngome ya upinzani.

AP/RTR

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW