1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

DRC na Uturuki zakubaliana kushirikiana kiusalama

21 Februari 2022

Rais Erdogan anajizatiti kuimarisha uhusiano na bara la Afrika katika nyanja mbali mbali ikiwemo usalama na biashara.

Kongo Kinshasa | Türkischer Präsident Erdogan trifft Präsident Tshisekedi
Picha: Turkish President Press Office/EPA-EFE

(Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan yuko ziarani barani Afrika, jana akiwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo alifikia makubaliano kadhaa ikiwemo ya usalama na rais Felix Tschisekedi.

Rais wa Jamhuri wa Kidemokrasi ya Kongo Felix Tschisekedi baada ya kukutana na kiongozi huyo wa Uturuki aliweka wazi kwamba wamefikia makubaliano yenye ushindi kwa pande zote mbili nchi yake na Uturuki. 

Katika ziara hiyo rasmi ya kiserikali ya siku mbili  iliyoitwa ya kihistoria nchini Kongo rais Recep Erdogan aliandamana na ujumbe wa maafisa wa serikali yake pamoja na wafanyabiashara.

Pamoja na mengine rais Tschisekedi amesema Kongo na Uturuki zimefikia makubaliano ya manufaa kwa pande zote mbili ambayo yatajenga ushirikiano kuhusu masuala ya usalama,miundombinu,afya pamoja na uchukuzi,lakini juu ya hilo rais huyo wa Kongo akaitaja jana kuwa ni siku ya kihistoria katika uhusiano kati mataifa hayo mawili baada ya kuzungumza na Erdogan.

Picha: Turkish President Press Office/EPA-EFE

Aidha rais Tschisekedi akaongeza kusema kwamba Kongo imeomba msaada wa Uturuki katika mapambano ya muda mrefu dhidi ya makundi la waasi katika eneo lenye mgogoro la mashariki .  Ziara hii ya Erdogan barani Afrika iliyoanza jana tarehe 20 mpaka 23  haishii tu nchini Kongo bali itamfikisha pia Senegal  na Guinea Bissau.

Ni ziara inayofuatia mikutano kadhaa baina ya  viongozi hao wawili mnamo mwaka jana. Mnamo mwezi Septemba,rais Tshisekedi alifanya ziara rasmi mjini Ankara,Uturuki akiwa na agenda ya kutafuta ushirikiano wa kiuchumi na nchi hiyo lakini pia alikwenda Istanbul mwezi Desemba mwaka jana alikoshiriki mkutano wa kilele baina ya Uturuki na Afrika.

Uhusiano baina ya Ankara na Kinshasa ni mzuri kwa kipindi cha miaka mingi na kiwango cha uwekezaji wa Uturuki nchini Kongo umeendelea kuongezeka. Na biashara kati ya pande hizo mbili imeongezeka na kufikia kiasi dola milioni 40 ingawa Uturuki inataka kujiimarisha zaidi katika bara la Afrika.

Ushawishi wa Uturuki Afrika 

Tangu mwaka 2003 kiwango cha biashara kati ya nchi hiyo na bara la Afrika kimeongezeka kutoka dola bilioni 2 mpaka kiasi dola bilioni 25. Na rais Erdogan ameshafanya ziara mara 40 barani Afrika tangu mwaka 2005 akiwa kama waziri mkuu na kisha kama rais na tangu wakati huo Uturuki imeshafungua balozi zake 40 katika bara hilo. Ushawishi wa Uturuki barani Afrika unajikita zaidi kwenye ulinzi ambapo imeshuhudiwa nchi hiyo ikianzisha kambi yake ya kwanza ya kijeshi barani humo mnamo mwaka 2017 nchini Somalia.

Erdogan akiwa Somalia 2016 kama waziri mkuuPicha: Kayhan Ozer/AA/picture alliance

Inafahamika kwamba Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo inakabiliwa na hali ya ukosefu wa usalama katika eneo lake la Mashariki kutokana na kuwepo makundi chungunzima ya waasi wenye silaha ambayo yanawatishia mara kwa mara raia.

Operehseni za kijeshi zinaendelea dhidi ya makundi hayo ikijumuisha lile linalojiita Allied Democratic Forces ADF,ambalo ni tawi la Dola la Kiislamu katika eneo hilo la Afrika ya Kati likilaumiwa kuhusika na mauaji ya maelfu ya watu mashariki mwa Jamhuri ya kidemokrasi ya Kongo.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri:Mohammed Khelef

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW