1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Erdogan aufungua Msikiti wa Cologne

Caro Robi
29 Septemba 2018

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amewasili mjini Cologne, Ujerumani Jumamosi kuufungua Msikiti mpya mjini humo unaosimamiwa na muungano wa makundi ya Kiislamu nchini Ujerumani na kufadhiliwa na Uturuki.

Deutschland Zentralmoschee Köln Ehrenfeld
Picha: picture-alliance/R. Hackenberg

Awali, maafisa wa Ujerumani walisema ratiba ya ziara ya rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan nchini Ujerumani ambayo Jumamosi ndio siku yake ya mwisho imebadilishwa kwa sababu za kiusalama na za kisiasa.

Mipango ya kuwa na mkutano wa hadhara katika msikiti huo imefututiliwa mbali na maafisa wa mji wa Cologne kwasababu za kiusalama na umma hautakubaliwa karibu na msikiti huo.

Ziara ya Erdogan yaibua hisia mseto

Hafla hiyo inaahudhuriwa tu na wageni waalikwa. Aidha Rais Erdogan atakutana na waziri mkuu wa jimbo la North Rhine Westphalia Armin Laschet katika uwanja wa ndege wa Cologne baada ya mmiliki wa kasri la Wahn ambako mkutano huo ulipaswa kufanyika kukataa kumpokea Erdogan akitaja sababu za kiusalama.

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan na Kansela wa Ujerumani Angela MerkelPicha: picture-alliance/dpa/J. Denzel

Laschet na Meya wa Cologne Henriette Reker wamekataa kuhudhuria hafla ya ufunguzi wa msikiti huo wa Cologne, unaotajwa kuwa miongoni mwa mikubwa zaidi barani Ulaya.

Msikiti huo mkubwa unasimamiwa na muungano wa makundi 900 ya Kiislamu yaliyoko Ujerumani ya Waturuki muungano ujulikanao DITIB. Pamoja na kuwa nyumba ya ibada, Msikiti huo utakuwa kituo cha mafunzo kwa Maimamu.

Taarifa iliyochapishwa katika ukurasa wa Facebook wa DITIB, imeelezea kusikitishwa na uamuzi wa baraza la jiji la Cologne ikisema inapinga hatua hiyo ya kufutilia mbali umma kuhudhuria hafla ya kufunguliwa kwa Msikiti huo na haioni sababu za kuchukuliwa hatua hizo. Hata hivyo DITIB imesema itafuata sheria.

Maelfu waandamana kumuunga na kumpinga Erdogan

Maelfu ya askari wametumwa Cologne kushika doria baada ya watu zaidi 25,000 kupitia ukurasa wa facebook wa Muungano huo wa makundi ya Kiislamu Ujerumani kusema watahudhuria sherehe hizo  na kuwafanya maafisa wa baraza la jiji kutafuta hakikisho kuhusu usalama kama njia za dharura iwapo kutatokea mkasa au upatikanaji wa maafisa wa afya kushughulikia dharura.

Waturuki wamiminika mitaani Cologne kumkaribisha ErdoganPicha: picture-alliance/dpa/C. Gateau

Erdogan anatarajiwa kutoa hotuba ya takriban dakika 20 msikitini humo itakayoangazia uhusiano kati ya nchi yake na Ujerumani na pia kuangazia kitisho kinachoongezeka ncha itikadi kali za mrengo wa kulia. Mawaziri kadhaa wa Uturuki pia wanahudhuria hafla hiyo.

Wakati huo huo huo, kiasi cha watu 1,000 wanaandamana mjini Cologne kupinga ziara ya Erdogan. Idadi hiyo ni ndogo ikilinganishwa na makadirio ya awali kuwa watu 10,000 walikuwa wanapanga kuandama dhidi ya Erdogan. Maelfu ya wafuasi wa Erdogan pia wamejitokeza katika mitaa ya Cologne wakipeperusha bendera na kumsifu kiongozi wao.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na Rais wa Ujerumani Frank Walter Steinmeier wameshutumu ukiukaji wa haki za binadamu unaofanyika Uturuki na walilijadili suala hilo na Rais Erdogan walipokutana katika ziara yake ya siku tatu Ujerumani.

Uhusiano kati ya Uturuki na Ujerumani katika miaka ya hivi karibuni umekuwa tete na ziara ya Erdogan ilitarajiwa kuboresha mahusiano hayo. Idadi ya Waturuki wanaoishi Ujerumani inakadiriwa kuwa zaidi ya milioni tatu. Merkel amesema kuna haja ya kuwa na mazungumzo ya kutatua tofauti zilizopo.

Mwandishi: Caro Robi/afp/dpa

Mhariri: Zainab Aziz

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW