1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Essebsi kuzikwa leo (27.07.2019)

27 Julai 2019

Viongozi wa ngazi za juu duniani wamewasili nchini Tunisia kushiriki kwenye ibada ya maziko ya rais wa kwanza aliyechaguliwa kidemokrasia aliyefariki alhamisi wiki hii.

Tunesiens Präsident Beji Caid Essebsi gestorben | Trauerfeier
Picha: Reuters/A. Awad

Viongozi wa ngazi ya juu duniani wameanza kuwasili nchini Tunisia Jumamosi (27.07.2019) kwa ajili ya maziko ya rais wa kwanza aliyechaguliwa kwa njia za kidemokrasia Beji Caid Essebsi.

Mfalme wa Qatar Tamim bin Hamad Al-Thani,rais wa mpito wa Algeria Abdelkader Bensalah na rais wa mamlaka ya wapalestina Mahmoud Abbas wameshafika mjini Tuni kwa ajili ya kushiriki kwenye ibada ya maziko yatakayofanyika chini ya usalama wa hali ya juu. 

Wawakilishi kutoka nchi zaidi ya 20 wanatarajiwa kushiriki kwa mujibu wa vyombo vya habari na vikosi vya usalama vimepelekwa katika maeneo yote ya mji mkuu Tunis kabla ya utaratibu wa maziko. Essebsi atazikwa baadae leo Jumamosi katika makaburi ya Tunis ambayo yako kiasi kilomita 7 kutoka yalipo makaazi ya rais.

Picha: Reuters/A. Awad

Maafisa wametangaza hatua ya kuzifunga barabara nyingi za mji mkuu wa Tunis kwa ajili ya shughuli hiyo ya safari ya mwisho wa rais Essebsi. Kiongozi huyo alikuwa na umri wa miaka 92 wakati wa kifo chake kilichomkuta siku ya alhamisi ikiwa ni miaka takriban mitano baada ya kuingia madarakani.

Katika kipindi chake yalishuhudiwa mashambulio kadhaa yaliyodaiwa kufanywa kwa kiasi kikubwa na kundi la magaidi la IS.Alichaguliwa kuiongoza Tunisia Desemba mwaka 2014 kukikamilisha kidemokrasia  kipindi cha mpito katika nchi hiyo baada ya vuguvugu la mapinduzi ya wananchi mwaka 2011 lililomuondowa madarakani mtawala wa kiimla Zine Ebadine Ben Ali aliyeitawala nchi hiyo kwa muda mrefu.

Tunisia iliyoko Kaskazini mwa Afrika  inaangaliwa kama nchi pekee iliyopata mafanikio ya kidemokrasia yaliyotokana na vuguvugu la wananchi lililokuja kupiga kwenye nchi nyingine za kiarabu,ingawa nchi hiyo imekuwa ikikabiliana na hali ngumu ya kiuchumi pamoja na vurugu zinazotokana na matatizo ya kijamii.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri:Sudi Mnette

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW