1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Felix Tshisekedi anasema muungano tawala hautovunjika

Saleh Mwanamilongo
17 Julai 2020

Rais Tshisekedi anatoa wito wa utulivu na mshikamano baina chama chake na kile cha mtangulizi wake Kabila.Tshisekedi anasema muungano tawala huo hautovunjika.

Rais wa Congo Felix Tshisekedi (Left) na mtangulizi wake Joseph Kabila,siku ya kuapishwa kwake mjini Kinshasa.
Rais wa Congo Felix Tshisekedi (Left) na mtangulizi wake Joseph Kabila,siku ya kuapishwa kwake mjini Kinshasa.Picha: Reuters/O. Acland

Rais wa Jamhuri wa Kidemokrasia ya Kongo,Felix Tshisekedi anatoa wito wa utulivu na mshikamano baina chama chake na kile cha mtangulizi wake Joseph Kabila. Tshisekedi anasema licha ya mikwaruzano lakini muungano huo hautovunjika.

Kwenye mkutano na wandishi habari kufuatia ziara yake ya siku moja mjini Brazzaville, huko Jamhuri ya Congo, rais Felix Tshisekedi anasema mvutano wa kisiasa ulioko hivi sasa nchini mwake utapatiwa ufumbuzi na hajafikiria kuvunjika kwa muungano tawala.

''Cha muhimu ni kutizama kwanza maslahi ya taifa. Kila upande unatakiwa kuwa makini kwa kuyapa kipaumbele maslahi ya nchi yetu. Tutamaliza kwa kupata suluhisho la mzozo wa hivi sasa. Nitakachowahakikishia ni kwamba muungano huo hautovunjika. Na wakati huu tunaozungumza kuna wajumbe wa pande zote mbili ambao wanajaribu kutafuta suluhisho''.

Msimamo huo wa rais Tshisekedi umekuja baada ya wiki kadhaa za kuwepo na hali ya kutoelewana katika muungano tawala juu ya mapendekezo yaliyotolewa na chama cha FCC cha rais Kabila, kilicho na wingi wa viti bungeni, kuweza kufanya mabadiliko ya idara ya sheria, hususan kuipatia nguvu zaidi wizara ya sheria katika kushughulikia mashitaka ya uhalifu.

Tofauti hizo zilisababisha wiki tatu zilizopita kukamatwa kwa muda mfupi, waziri wa sheria na kusababisha waziri mkuu kutishia kujiuzulu kwa serikali. Viongozi wote wawili wanatoka chama cha FCC cha Kabila.

Congo bado ni demokrasia changa

Rais wa Congo Felix Tshisekedi atoa mwito wa utulivu katika muungano tawala.Picha: G. Kusema

Katika hotuba yake kwa taifa ya kuadhimisha miaka 60 ya uhuru wa Congo kutoka mikononi mwa Ubelgiji,Juni 30, Tshisekedi aligusia mgogoro huo, akisema hakubaliani na mageuzi yoyote.Wiki iliyopita,wafuasi wa rais Tshisekedi waliandamana mjini Kinshasa ili kupinga mswada huo wa sheria kutoka kwa wabunge wa FCC na pia uteuzi wa kiongozi mpya wa tume ya uchaguzi. Hata hivyo rais Tshisekedi anaamini kwamba sio rahisi kuweko na maelewano kuhusu maswala nyeti.

''Hali hii inatokana na kwamba bado Kongo ni demokrasia changa.Ni mfano wa kwanza wa kisiasa nchini mwetu,kuhusu muungano wetu.Hata katika nchi zenye demokrasia kongwe mikwaruzano ya kisiasa ipo.Kwa hiyo tusiwe na wasiwasi kuhusu yanayotokea hivi sasa''alisema Tshisekedi.

Rais Tshisekedi ambaye amekuwa madarakani kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa, aliingia katika maelewano na chama cha FCC cha rais wa zamani,Joseph Kabila,kushirikiana naye katika serikali yake,baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2018.

Kabila bado ana nguvu kupitia wingi wa viti bungeni, baraza la mawaziri na ofisi ya waziri mkuu.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW