Rais Ghani kukutana na kansela Merkel Berlin
2 Desemba 2015Mazungumzo kati ya viongozi hao yatajikita zaidi juu ya mzozo wa sasa wa wakimbizi. Tayari zaidi ya raia 140,000 wa Afghanistan wamekimbilia Ulaya mwaka huu, wengi wao wakikamilisha safari zao na kupewa hifadhi Ujerumani.
Kwa mujibu wa Ofisi ya Shirikisho inayohusika na masuala ya wakimbizi, Ujerumani iliwaorodhesha watu zaidi ya 31,000 walioomba hifadhi kutoka Afghanistan. Hii inawafanya Waafghani kuwa kundi la pili kubwa la wakimbizi baada ya Wasyria.
Lakini Ujerumani inayakataa zaidi ya nusu ya maombi ya uhamiaji yaliyowasilishwa na raia wa Afghanistan. Serikali tayari imeshasema haiwezi kuyakubali maombi yote na kwamba wakimbizi wanaoshindwa kupata uhamiaji watarejeshwa nchini kwao.
Ubalozi wa Ujerumani mjini Kabul umezindua kampeni ya kusambaza taarifa kufuta uvumi unaoenea miongoni mwa Waafghani kwamba ni rahisi kupata uhamiaji nchini Ujerumani. Ndio maana mzozo wa wakimbizi utakuwa mada muhimu katika mazungumzo kati ya Merkel na Ghani.
Wiki iliyopita jarida la Ujerumani la Der Spiegel lilinukuu ripoti ya ndani kutoka kwa ubalozi wa Ujerumani mjini Kabul iliyosema utanuzi wa kundi la Taliban ni mkubwa leo kuliko wakati wa kuanza kwa ujumbe wa jumuiya ya kujihami ya NATO nchini Afghanistan mwaka 2001.
Ripoti inasema hali hiyo hivi karibuni itasababisha ongezeko la maombi halali ya uhamiaji. Wakati huo huo, serikali ya Afghanistan inazuia kurejeshwa kwa wahamiaji walionyimwa vibali vya uhamiaji.
Msemaji wa rais Ghani, Sayed Zafar Hashemi, ameiambia DW kwamba wanafanya kila wawezalo kuhakikisha Waafghani hawahisi ni muhimu kuihama nchi yao.
Msemaji huyo aidha amesema, "Tunajaribu kuwasaidia walioamua kuondoka Afghanistan na ambao maombi yao ya uhamiaji yalikataliwa, lakini kuna mipaka."
Wizara ya mambo ya nje ya Ujerumani inatishia kupunguza msaada wa maendeleo kwa Afghanistan iwapo mipaka hiyo haitashughulikiwa.
Usalama wa Afghanistan kujadiliwa
Suala jingine litakalokuwa katika ajenda ya mazungumzo kati ya Kansela Merkel na Rais Ghani ni kuzorota kwa hali ya usalama nchini Afghanistan. Mbali na kitisho kinachosababishwa na kundi la Taliban, lililofaulu kuudhibiti mji wa Kunduz wiki chache zilizopita, sasa kuna kitisho kipya.
Makundi tiifu kwa kundi la Dola la Kiislamu IS yanatanua ushawishi wao, hususan katika eneo la mashariki la nchi. Mwezi uliopita maelfu ya watu walijitokeza mabarabarani kuandamana mjini Kabul kufuatia kuchinjwa vichwa na kuuliwa kwa wafuasi wa madhehebu ya Shia walio wachache Afghanistan. Waandamanaji hao walimlaumu Rais Ghani kwa kushindwa kuulinda umma.
Ziara ya Rais Ghani mjini Berlin inakuja wakati Ujerumani na Afghanistan zikiadhimisha miaka 100 ya urafiki. Oscar Niedermayer, afisa wa jeshi la Ujerumani aliyeongoza msafara wa Wajerumani kwenda Afghanistan mwaka 1915, hangefikiria kwamba karne ingekamilika wakati kukiwa na wimbi kubwa la raia wa Afghanistan wakihamia Ujerumani.
Safari ya Niedermayer-Hentig ilikuwa mkakati wa kuiweka Afghanistan upande wa himaya ya Ujerumani wakati wa vita vya kwanza vya dunia. Karne moja baadaye Waafghani wengi bado wanatumia uhusiano huu wanapoondoka kwao kuja kujaribu bahati yao Ujerumani.
Mwandishi: Hasrat-Nazimi, Waslat
Tafsiri: Josephat Charo
Mhariri: Caro Robi