Bush aiunga mkono Ukraine kujiunga na NATO
1 Aprili 2008
Rais George W. Bush wa Marekani yupo nchini Ukraine katika ziara yenye lengo la kuiunga mkono nchi hiyo inayokusudia kujiunga na jumuiya ya kijeshi ya NATO.
Rais Bush anaefanya ziara nchini Ukraine amesema anaunga mkono thabiti lengo la nchi hiyo la kuwa mwanachama wa mfungamano wa kijeshi - NATO. Rais Bush amesema ataweka mkazo juu ya suala hilo kwenye mkutano wa viongozi wa nchi za NATO utakaoanza kesho mjini Bucarest Rumania. Amesema atawataka viongozi wengine wa NATO waunge mkono maombi ya Ukraine na Georgia ya kujiunga NATO.
Wakati huo huo rais Bush ameonya kuwa Urusi haitakuwa na kura ya veto kwenye mkutano wa nchi za NATO ambapo viongozi wa jumuiya hiyo ya kijeshi wataamua juu ya kuwaingiza wanachama wapya.
Rais Bush ametoa kauli hiyo kufuatia onyo lililotolewa na Urusi juu ya Ukraine inayokusuddia kujiunga na jumuiya ya NATO.Urusi imesema ikiwa Ukraine itajiunga na NATO, hatua hiyo itasababisha mgogoro mkubwa katika uhusiano baina ya nchi hiyo na Urusi.
Naibu waziri wa mambo ya nje wa Urusi Grigory Karasin amekaririwa na mashirika ya habari akisema,ikiwa Ukraine itaingizwa katika NATO,hatua hiyo itaathiri usalama wa bara la Ulaya
Naibu waziri huyo amezitaka nchi za magharibi ziamue , ni aina gani ya uhusiano zinata uwepo baina yao na Urusi.
Hatahivyo rais Viktor Yushenko wa Ukraine amesema nchi yake inatumai kupata ishara nzuri kutoka kwa viongozi wa nchi za NATO watakaokutana kuanzia kesho mjini Bucarest, Rumania.
Wadadisi wanasema kauli ya rais Yushenko itasababisha mvutano zaidi baina ya Urusi na nchi za magharibi.
Viongozi wa nchi za NATO wanatarajia kuamua juu ya uanachama wa Ukraine kwenye mkutano wa wa kesho mjini Bucarest.