Rais Hassan Rouhani wa Iran yuko ziarani Ulaya
25 Januari 2016Katika kinyang'anyiro cha kuania mikataba,lilikuwa kampuni la ndege la Airbus lililokuwa la mwanzo; jumamosi iliyopita waziri wa usafiri wa Iran alitangaza azma ya Iran kununua ndege 114,mkataba ambao rais Rouhani anapanga kuutia saini atakapokuwa ziarani mjini Paris jumatano ijayo. Lilikuwa tangazo la mwanzo kubwa la kibiashara tangu vikwazo vya kimataifa vilipoondolewa rasmi january 16 iliyopita.
Katika ziara hii rasmi ya siku nne,rais Hassan Rouhani amepangiwa kukutana na waziri mkuu wa Itali Matteo Renzi na baadae kiongozi wa kanisa katoliki Papa Francis kabla ya kwenda Ufaransa kwa mazungumzo pamoja na rais Francois Hollande.
Itafaa kusema hapa kwamba ziara ya rais Rouhani nchini Ufaransa ilipangwa kwanza mwezi wa Novemba,kabla ya kuakhirishwa kufuatia mashambulio ya kigaidi ya Paris.
Kabla ya kuondoka Iran,rais Rouhani alisema atatiliana saini makubaliano muhimu pamoja na Itali na Ufaransa, makubaliano yatakayofungua njia ya kuanzishwa uhusiano wa muda mrefu pamoja na nchi za Ulaya."Nataraji ziara hii itakuwa ya maana kwa nchi yetu,kiuchumi,kitamaduni na kiteknolojia.Tunabidi tuyatumie makubaliano ya baada ya mvutano wa mradi wa nuklea kwaajili ya kuhimiza ukuaji wa kiuchumi,maendeleo ya nchi yetu na kjubuni nafasi za kazi kwa vijana wetu. Ziara hii inaambatana na lengo hilo."
Rais Rouhani atakutana kwa mazungumzo na kiongozi wa kanisa katoliki ulimwenguni Papa Francis
Mjini Roma,rais Hassan Rouhani amepangiwa kukutana kwanza na kiongozi mwenzake Sergio Mattarella.
Vatikan inasifu msimamo wa wastani unaofuatwa na Iran tangu Hassan Rouhani alipochaguliwa kuwa rais. Duru zinasema kiongozi wa kanisa katoliki anapanga wakati wa mazungumzo yake pamoja na rais Rouhani,kuzungumzia kuhusu mchango wa kutuliza hali ya mambo unaoweza kutolewa na Iran Mashariki ya Kati na kumsihi asaidie kupunguza mvutano pamoja na Riyadh pamoja pia na kumshinikiza rais wa Syria Bashar al Assad.
Kesho rais Rouhani amepangiwa kuhutubia kongamano la kiuchumi la Iran na Italy-tukio linalosubiriwa kwa hamu kubwa na wanaviwanda wa Itali.
Wajasiria mali wasiopungua 500 wa Itali wanatarajiwa kuhudhuria kongamano hilo kesho asubuhi.
Rais Hassan Rouhani anafuatana na ujumbe mkubwa ,wakiwemo viongozi mia moja wa kiuchumi,pamoja na waziri wa mambo ya nchi za nje,waziri wa mafuta ,usafiri,viwanda na afya.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP
Mhariri:Yusuf Saumu