1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Joachim Gauck nchini Ufaransa

Abdu Said Mtullya4 Septemba 2013

Marais wa Ujerumani Joachim Gauck na wa Ufaransa Francois Hollande wamekitembelea kijiji cha Oradour sur -Glane nchini Ufaransa ambako mafashisti wa kijerumani walifanya mauaji halaiki wakati wa vita kuu vya pili.

Marais Gauck na Hollande katika cha Oradour-sur-Glane
Marais Gauck na HollandePicha: REUTERS

Joachim Gauck anaendelea na ziara ya nchini Ufaransa ,ni Rais wa kwanza wa Ujerumani kuenda kwenye kijiji hicho. Ziara ya Rais wa Ujerumani kwenye kijiji hicho ni ishara ya maridhiano baina ya Ujerumani na Ufaransa.

Kijiji hicho kilikuwa mahala ambako mafashisti wa kijerumani waliwaua raia 620 mnamo mwaka wa 1944.Theluthi moja ya watu waliouawa walikuwa watoto. Askari wa Ujerumani kwanza walikizingira kijiji hicho na baadae waliwaswaga watu hao na kuwapeleka katika soko moja. Wanaume walipigwa risasi ndani ya ghala, na wanawake na watoto walifungiwa ndani ya kanisa la kijiji lililopigwa moto na mafashisti.

Rais Gauck aonyesha mshikamano

Manazi walikipiga moto kijiji baada ya kuwaangazamiza watu hao.Muda mfupi kabla ya kwenda kwenye kijiji hicho Oradour sur -Glane Rais wa Ujerumani Joachim Gauck aliiambia radio ya "Europa 1" kwamba madhumuni ya ziara yake ni kuonyesha mshikamano na waliofikwa na maafa ya mafashisti .Katika ziara yake Rais Gauck amekutana na watu walionusurika maangamizi ya mafashisti.

Viongozi wakionesha mshikamo wa dhatiPicha: picture-alliance/dpa

Rais wa Ujerumani aliefuatana na Rais wa Ufaransa Francois Hollande kwenye kijiji cha Oradour sur-Glane amesema anajua kilichofanyika na ndiyo sababu aliukubali mwaliko akiwa na mgawanyiko wa hisia;shukurani na unyenyekevu.Hata hivyo Rais wa Ujerumani amesema hatachoka kutumia kila wasaa kueleza kuwa Ujerumani sasa imebadilika.

Mgogoro wa Syria katika ajenda

Bwana Gauck anafanya ziara ya situ nchini Ufaransa wakati ambapo mgogoro wa Syria unagonga vichwa vya habari. Juu ya mgogoro huo, Rais huyo wa Ujerumani amesema panahitajika jibu linalostahili. Amesema ameenda Ufaransa na salamu za dhati ya moyo kutoka kwa Kansela Merkel anaetumai kwamba pakitokea fursa yoyote, kama kwenye mkutano wa kilele wa viongozi wa nchi za G20, suala la Syria litajadiliwa na kufikiwa makubaliano ya kimataifa yatakayokuwa jawabu sahihi kwa Syria. Rais wa Ujerumani pia amesitiza kwamba suala la Ujerumani kushiriki katika kuishambulia Syria halimo katika ajenda.

Shida zinazowakabili watu wa Syria kila sikuPicha: Reuters/Goran Tomasevic

Miaka 50 ya maridhiano

Bwana Gauck alianza ratiba yake leo kwa kuweka shada la maua kwenye kaburi la askari asiyejulikana kwenye kumbukumbu ya mjini Paris ya vita kuu vya kwanza. Ziara ya Rais Gauck nchini Ufaransa inazingatiwa kuwa muhimu sana,kwani inafanyika katika maadhimisho ya mwaka wa hamsini wa mkataba wa Elysee ulioleta maridhiano baina ya Ujerumani na Ufaransa.

Rais Gauck mwenye wadhifa wa heshima alipewa heshima kamili za kijeshi alipowasili mjini Paris jana kuanza ziara yake ya Ufaransa. Hapo jana pia alikuwa na mazungumzo ya kwanza na mwenyeji wake Rais Francois Hollande .Rais Gauck anatarajiwa kumaliza ziara yake ya nchini Ufaransa hapo kesho kwa kuutembelea mji wa bandari wa Marseille ambao mnamo mwaka huu umeazimiwa kuwa mji wa utamaduni barani Ulaya.

Mwandishi:Mtullya Abdu/dpa
Mhariri: Josephat Charo