1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Biden ajitetea juu ya kufanya ziara nchini Saudi Arabia

11 Julai 2022

Rais wa Marekani atafanya ziara katika eneo la Mashariki ya Kati wiki hii na moja kati ya nchi atakazo kwenda ni Saudi Arabia. Biden yuko tayari sasa kukutana na viongozi wa Saudi Arabia na anaitetea ziara yake hiyo.

 Joe Biden und Sultan bin Abdul-Aziz Al Saud
Picha: Hassan Ammar/AP/picture alliance

Rais wa Marekani Joe Biden katika ziara yake hiyo kwenye eneo la Mashariki ya Kati atakwenda nchini Israel siku ya Jumatano, ila macho yote yanakodolea safari ya kiongozi huyo wa Marekani ya mjini Jeddah, nchini Saudi Arabia mnamo siku ya Ijumaa.

Miongoni mwa kauli za Biden alipokuwa mgombea urais, alisema mauaji ya mwaka 2018 ya mwandishi Habari Jamal Khashoggi wa gazeti la Washington Post huko nchini Uturuki kunaifanya Saudi Arabia kuwa ni taifa linalopaswa kutengwa na jumuiya ya kimataifa na kwamba atahahikikisha kuwa hilo linafanyika, aliilaumu Saudi Arabia kwa kukosa utu na kuwa kinara wa kuvunja haki za binadamu.

Rais wa Marekani Joe BidenPicha: picture alliance / ASSOCIATED PRESS

Mara baada ya kushinda uchaguzi, utawala wa Biden ulichapisha matokeo ya kijasusi ambayo yalimbainisha kiongozi, ambaye ni mrithi wa mfalme wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman, kama muhusika mkuu aliyepanga operesheni ya kuuliwa kwa Jamal Khshoggi. Lakini sasa hali imebadilika na rais Biden anaonekana kuwa yuko tayari kushirikiana tena na Saudi Arabia nchi ambayo imekuwa mshirika mkuu wa kimkakati wa Marekani kwa miongo kadhaa, pia msambazaji mkuu wa mafuta na mnunuzi wa silaha za Marekani.

Mwelekeo wa rais wa Marekani wa hivi karibuni umebadilika na kuwa ni wa kuipongeza Riyadh kwa juhudi za kuvimaliza vita nchini Yemen.

Gazeti la The Washington Post

Biden amesema katika makala yake aliyoandika kwenye gazeti la Washington Post la nchini Marekani kwamba sera yake ya nje imelifanya eneo la Mashariki ya Kati liwe imara na salama zaidi kulinganisha na hali ilivyokuwa wakati wa utawala wa rais wa hapo awali Donald Trump. Ameeleza kuwa ziara yake vilevile inahusiana na uvamizi wa Urusi nchini Ukraine na pia mashindano na China ambapo amesema Saudi Arabia inaweza kutoa mchango muhimu.

Kiongozi huyo wa Marekani amesema anafahamu kuwa wapo wengi ambao hawakubaliani na uamuzi wake wa kusafiri kwenda Saudi Arabia lakini amesisitiza kuwa msimamo wake juu ya maswala ya haki za binadamu unaeleweka wazi, na ni wa kimsingi.

Mwandishi Habari Jamal Khashoggi wa gazeti la Washington Post aliyeuawa huko nchini Uturuki Picha: Yasin Ozturk/AA/picture alliance

Jon Alterman, makamu wa rais katika Kituo cha Mafunzo ya Kimkakati na maswala ya Kimataifa (CSIS) cha mjini Washington, amesema utawala wa Biden umegundua kile ambacho tawala zote za Marekani zimekuwa zinakizingatia kwa miongo kadhaa, kwamba kufanikiwa kwa mambo mengi katika eneo la Mashariki ya Kati na kote ulimwenguni kunakuwa rahisi ikiwa Saudi Arabia inahusishwa na mambo yanakuwa magumu ikiwa taifa hilo halisaidii.

Kwenye Makala yake, Biden amesema Saudi Arabia inashirikiana na wataalam wa Marekani katika kuleta utulivu kwenye soko la mafuta. Alterman amesema Marekani inamtaka muuzaji huyo mkubwa zaidi wa mafuta ghafi duniani kuongeza uzalishaji wa bidhaa hiyo ili kupunguza bei ya petroli inayopanda kila uchao na ambayo inatishia nafasi ya kushinda kwa chama cha Democratic cha rais Biden katika uchaguzi wa mwezi Novemba.

Mrithi wa mfalme wa saudi Arabia Mohammed bin SalmanPicha: Saudi Royal Court/REUTERS

Ikulu ya Marekani inazingatia umuhimu wa safari ya rais Joe Biden na kukutana na mrithi wa mfalme maarufu kwa jina MBS, ambaye atakuwa ni sehemu ya wajumbe wakati Biden atakapofanya mazungumzo na Mfalme wa Saudi Arabia Salman bin Abdel-Aziz.

Vyanzo:AFP/ https://p.dw.com/p/4DvWo

Mhariri:

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW